Sep 22, 2010

UZINDUZI WA TAMKO LA WANAHARAKATI WASIO WA KISERIKALI 2010; “WAKATI NA BAADA YA UCHAGUZI2010"

Asasi ya Agenda Participation 2000 asasi isiyo ya kiserikali inayofanya kazi ya kuhamasisha utamaduni wa utawala bora na demokrasia ndani ya Tanzania. Asasi pamoja na mambo mengine inatoa elimu ya uraia, mafunzo na kuhifadhi masuala ambayo yanaweza kuimarisha ushiriki wa wananchi katika utawala, demokrasia na michakato ya maendeleo.

AP2000, ikiongozwa na Dira ya; “Kuona jamii ya kidemokrasia na yenye amani na dola au nchi inayoendeshwa na utamaduni wa misingi au kanuni za kidemokrasia”. AP2000 imekuwa ikiratibu tangu mwaka 2005 na pia mwaka huu 2010 mchakato wa kukusanya na kuboresha maoni ya wanaharakati wasio wa kiserikali katika masuala mbali mbali nyeti kwa maslahi ya Taifa letu.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, AP2000 imehusika kuratibu uandaaji wa Tamko la Wanaharakati Wasio wa Kiserikali kwa msaada wa mashirika mbalimbali kwa taarifa na ushauri. Sambamba na mashirika hayo, kwa namna ya pekee Shirika la Kijerumani la Friedrich Ebert Stiftung, wamehusika kufadhili uchapaji, uzinduzi na usambazaji wa tamko hili.

Tamko la Wanaharakati Wasio wa Kiserikali tunalolizindua leo kupitia mgeni rasmi Mhe. Jaji Mstaafu Lameck Mfalila, 21.09.2010 katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar-es-Salaam likishuhudiwa na wanaharakati toka Asasi za kiraia, Balozi, Mashirika ya Kimataifa, Wanahabari, na wananchi wote kwa ujumla toka kila pembe ya Tanzania limegusa maeneo makuu yafuatayo;

  1. Tathmini ya Maendeleo Kiuchumu na Haki
  2. Ajira
  3. Mazingira na Maliasili
  4. Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
  5. Huduma za Jamii
  6. Uongozi na Utawala
  7. Rushwa
  8. Maisha na Usalama wa Binadamu
  9. Maadili ya Uchaguzi

Vipaumbele hivi vilivyofafanuliwa kwa kina sana katika chapisho la Tamko hili, vinaangaliwa na Wanaharakati Wasio Wakiserikali kama msingi wa kupiga kura wagombea kutoka vyama vya siasa. Sambamba, kuwataka wagombea ngazi za Udiwani, Ubunge na Urais pia viongozi na watumishi wa umma kuzingatia maazimio hayo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2010.

Maazimio haya yanabeba uzito na masuala nyeti yanayoikandamiza Taifa na kuzidi kuliweka katika hali ngumu na kikwazo kuelekea ustawi na maendeleo endapo hayatashughulikiwa kwa haraka na kiukamilifu

Uchaguzi Mkuu unatoa nafasi adhimu kwa wapiga kura na wagombea kukumbuka malengo ya msingi ya mfumo wa uchaguzi, yaani kuweka mbele na kulinda maslahi ya Taifa hili. Kwa mantiki hiyo, tunasisitiza uwepo wa mchakato wa uchaguzi wenye uwazi, haki na amani.Lakini pia, tunapinga vikali aina yoyote ya vitisho, rushwa, mizengwe au hila kupindisha ushindi utokanao na kura halali za wananchi.Tunasisitiza katika siasa safi zenye kuzingatia misingi ya kidemokrasia.

Haya ndiyo tunayoyaamini, tunayoyasimamia, tuna amini yana msingi sasa na hata baada ya Uchaguzi Mkuu 2010. Wagombea watakaoingia madarakani, viongozi wa umma wote wanapaswa kuyasimamia kwa vitendo kwa maslahi na ustawi wa Taifa letu.

Tanzania tunayotaka kuiona ni Taifa lenye amani na maendeleo ambalo linaheshimu haki za wananchi

wake wote bila kujali jinsia, hadhi, dini, kabila, imani ya kundi fulani na uwezo kimwili ama kiuchumi. Tunataka Tanzania ambayo licha ya kutokuwa na wala rushwa, inaendeshwa na viongozi wenye uvumilivu na uadilifu, wenye kutumia ipasavyo maliasili na rasilimali hususan watu. Tunataka Tanzania inayojitosheleza kwa chakula; yenye miundombinu bora yenye misingi ya kiteknolojia; na yenye kutafsiri maendeleo ya kitaifa kwa kuangalia afya, elimu na ustawi wa jamii. Tunaomba wananchi wote wayasimamie haya na kuyafatilia, kwa sababu Tanzania tunayotaka inawezekana.

Ninawashukuru sana kwa kufika kwenu katika uzinduzi huu. Ni matumaini yangu makubwa mtaupasha umma vizuri juu ya haya tuliyowasilisha kwa umma kupitia tamko hili.

Mungu Ibariki Tanzania!

Imetolewa na;

Your browser may not support display of this image. Prof. Max Mmuya,

Mwenyekiti, Agenda Participation 2000.

Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete mkoani Kilimanjaro

Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete wa pili(kulia) akisalimia wakati alipowasili Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro na kufanya mkutano wa ndani kwa wanachama wa UWT jimboni kuhusu umuhimu wa kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 31, mwaka huu kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu. (kulia) Mgombea Ubunge Jimbo la Mwanga Prpf. Jumanne Magembe, akifuatiwa na Mwenyekiti wa UWT Mkoa Kilimnjaro Regina Chonjo. Picha na Mwanakombo Jumaa.
Mama Salma Kikwete akimnadi mgombea ubunge jimbo la Mwanga Mkoa Kilimanjaro Prof. jumanne Magembe
Mama Salma Kikwete akimnadi Mgombea ubunge (CCM) Jimbo la Same Magharibi David Mathayo
Wakina mama wa UWT mjini Moshi wakishangilia wakati mama Salma alipoongea nao katika mkutano wa ndani
Wakina Mama wa Wilaya ya Mwanga wakimsikiliza mama Salma Kikwete wakati alipowahutubua kwenye mkutano wa ndani akielezea umuhimu wa kupiga kura kwa mwanamke.

DR. JAKAYA KIKWETE AENDELEA NA KAMPENI MKOANI IRINGA

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi CCM Jakaya Mrisho Kikwete akimnadi mgombea ubunge jimbo la Isimani William Lukuvi ambaye amepita bila kupingwa baada ya kukosa mpinzani katika mikutano mbalimbali ya kampeni iliyofanyika jana mkoani Iringa. Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu nchini kote. (Picha kwa hisani ya Akal Issa Michuzi).
Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa Iringa mjini Bw. Frederick Mwakalebela kwa pamoja wakiwasalimia wananchi waliofika kwenye mkutano wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Samora mkoani Iringa. Mwakalebela, huku akishangiliwa na maelfu ya wakazi wa mji huo, aliweka historia ya kuwa mwana CCM aliyenadiwa hadharani pamoja na kushindwa katika kura za maoni ambapo alipopanda jukwaani sio tu alitangaza kuvunja makundi bali pia kuomba wananchi wa Iringa kumpa kura mshindani wake Mh. Monica Mbega na madiwani pamoja na Rais kwenye uchaguzi mkuu Octoba 31.
Aliyekuwa mbunge wa Sumbawanga Mjni mzee Paul Kimiti akiwa katika picha ya pamoja na Mgombea wa jimbo la Iringa Mjini Monica Mbega kushoto na aliyekuwa mgombea wa CCM katika kura za maoni ndani ya chama Fredirick Mwakalebela jana wakati Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alipofanya ziara mkoani humo na kuhutubia mikutano mbalimbali ya kampeni.
Umati mkubwa ukiwa umjeaa kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa wakati Dr. Jakaya Kikwete alipohutubia kutano mjini humo.
Huu ndiyo umati wa baadhi ya watu aliohudhuria kwenye mkutano mgombea wa CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete jana kwenye uwanja wa Samora.

HUU NDIYO USAFIRI WA MOHAMMED DEWJI MGOMBEA UBUNGE SINGIDA MJINI!!

Huu ndiyo usafiri wa mgombea ubunge wa jimbo la Singida Mjini Bw. Mohammed Dewji hapa kama unavyomuona akiwa amepozi kwa picha mbele ya usafiri wake. (Picha kwa hisani ya Mo Blog)
Mchuma ukiwa tayari kwa kazi moja tu ya kumsafirisha mgombea wa ubunge jimbo la Singida kupitia Chama cha Mapinduzi CCM kila kona ya jimbo hilo katika mikutano yake ya kampeni.

Buriani Dk. Ernest Mashimba!!

Na Barnabas Lugwisha

Jumapili usiku, mida ya saa mbili hivi Mwandishi mwenzangu wa Habari , Mbaraka Islam, alinipigia simu na kuniuliza, “kaka umesikia kwamba Dk.Mashimba amefariki,” nikamwabia sijui kwa kweli, akasema hebu fuatilia, nikawapigia simu Wahariri watatu Absolom Kibanda, John Mapinduzi na Jackson Manyerere nikapata hakikisho.

Ni kweli ametutoka msomi huyu na kazi ya Mungu haina makosa, alikuwa mtu asiye na majivuno, mpenda utani na pande la baba kama ilivyo kwa wanaume wengi wa kisukuma.

Kabla ya umauti kumfika, alinusurika kifo mwanzoni mwa miaka ya 2000 maeneo ya Chango’mbe ambapo dereva wake alifariki hapo hapo, ilikuwa ni ajali ya kugongana na nadhani na daladala.

Alitibiwa na akapona, alivyokuwa muhimbili amelezwa alipata fahamu na kuagiza wasaidizi wake wanipe maelekezo kwamba niandike stori ambayo itaonyesha kwamba anaendelea pia nilizungumza naye kwa simu na akaniambia “Lugwisha, waambie wananchi sijafa, niko hai, kaandike hivyo poti,” kweli nikaandika hivyo akafurahi sana, baadaye alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na akapona.

Dk. Mashimba hakuwa na mbwembe kama ilivyo kwa wasomi wengi wa ngazi yake, ambao wengi wao huwa na mikogo na kujifanya Miungu watu kana kwamba hawatauonja umauti.

We fikiria wakati mwingine nilikuwa nakunywa naye supu ya utumbo pale Chuo Cha Usimamisi wa Fedha (IFM), nani mwenye nafasi kama yake atafanya hivyo, wengi hujiona miungu watu, kwa Dk Mashimba haikuwa hivyo na simpambi kwa kuwa ametangulia mbele ya haki, alikuwa ni mtu wa watu ,ni nadra sana kumuona amevaa suti, labda kuwe na ugeni mzito kwake.

Mwaka 2005 niliandika makala yake moja yenye kichwa “Mkemia Mkuu Asiyevaa” suti, nilidhani atakasirika lakini, kumbe alifurahi sana , akaikata ile makala na kuibandika kwenye ubao wa matangazo pale nje ya ofisi yake.

Nilifahamiana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1997 nikiwa Mwandishi wa The African maeneo ya Idara ya Habari Maelezo nakutana, nakumbuka ilikuwa ni kwenye mkutano wa Waandishi wa Habari, wakati huo Dr Mashimba alikuwa ameambatana na Waziri wa Afya wa wakati huo, Dr Aron Chiduo.

Ndani ya Mkutano huo nilimbana bana na maswali Dr Mashimba ambaye alikuwa akimsaidia Dk Chuduo kutoa ufafanuzi masuala mbalimbali.

Tulipomaliza Mkutano huo Dr Mashimba alinialika Ofisini kwake pale jirani na Hospitali ya Ocean Road na kuanza kufahamiana naye na kasha nikawa nafanya kazi za Uhusiano wa Umma za Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa takriban miaka saba hivi.

Kilichonivutia katika historia ya Dk Mashimba ambaye leo hatunaye ni historia ya maisha yake , ni Msukuma wa Ngudu, Kwimba lakini amesomea Zanzibar kuanzia Darasa la kwanza hadi alipojiunga na chuo kikuu Cha Dar es Salaam mwazoni mwa miaka 1980, kabla serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijampeleka nchini Australia kwa masomo ya ya shahada ya Pili na shahada ya Uzamivu (PHD).

Alivyorudi nchini kutoka ughaibuni mwaka 1995 , alipandishiwa cheo na kuwa Mkemia Mkuu wa Zanzibar, japo alikuwa amekaa Zanzibar tangu utoto wake lafudhi yake haikubadilika, ilikuwa ni ya Kisukuma tu, mwaka 1996 iliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuwa Mkemia Mkuu wa Zanzibar alikuwa akiendesha daladala, nilimuuliza kuhusu ukweli huo alikubali.

“Ndiyo poti kwani nikiendesha daladala kuna nini, si ya kwangu bwana”, alisema huku akicheka.

Tukiaachana na hayo, atakumbukwa kwa kufanya mambo mengi pale Maabara ya Mkemia Mkuu, chini ya utawala wake, maabara iliboreshwa, aliwezesha mashine ya DNA kununuliwa na alijenga Maabara ya Kanda pale Mwanza.Alikuwa ni mchapa kazi kwelikweli.

Alitupeleka kozi mbalimbali baadhi ya Waandishi wa Habari zihusuzo maswala ya Maabara yake na kwa kweli huduma mbalimbali ziliboreshwa na kuuzingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao kwake yeye ndiyo ilikuwa ilani ya utendaji wake.

Aliiboresha Maabara kwa vifaa mbalimbali vya kisasa muda mwingi alikuwa akiwahurumia wachimbaji madini wadogo wadogo wanaotumia madini ya Mercury kusafishia madini yao .

Alianzisha huduma za elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa kupima maji ya visima kwenye maabara yake kwali aliamini kwamba visima vingi vya maji ya kunywa hapa jijini si salama,.

Nilimshawishi kuanzisha jarida la Elimu ya Ukemia kwa Umma, alikubali na nikapata bahati ya kuwa muhariri wa kwanza jarida hilo , kwa kufanya kazi kwa karibu na Dk.Mashimba nilipata nafasi ya kujifunza mambo mengi ya yahusiyo tasnia hiyo muhimu ya Ukemia hapa nchini.

Nakumbuka kuna wakati ilitokea mvutano baina ya serikali ya mapinduzi Zanzibar na Muungano, Zanzibar walitaka akafanye kazi kwao kwa kuzingatia kwamba serikali ya mapinduzi ndiyo iliyomsomesha.

Amefariki akiwa usingizini, ilikuwa ni mipango ya Mungu, ametangulia na sisi tuko nyuma yake.

Ulale Mahale pema peponi Dk. Mashimba.

Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya yatoa msaada wa kompyuta kwa Asasi ya Guluka Kwalala leo jijini dar


Mkemia Mwandamizi wa wa Tume,Bw. Yovin Ivo (kulia) akiongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo wakati wa kukabidhi msaada wa Kompyuta ikiwa pamoja na Hp Laser jet P2055 Printer, APC Back-ups 650VA na Kasperky Antivirus 2010 Licensed, yenye thamani ya Tsh. 2,643,500/=.kwa Asasi ya Guluka Kwalala inayoshirikiana na Tume kukabiliana na kudhibiti matumizi wa dawa za kulevya nchini. kushoto ni Afisa Mtumishi Mkuu wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya,Bi. Aida Tesha
Katibu Mtendaji wa Asasi ya Guluka Kwalala,Bw. Bernard Ndunguru akitoa maelezo kwa vyombo vya habari namna wanavyokabiliana na matumizi ya dawa za kulevya pia alitoa shukrani kwa tume juu ya msaada walioupata na kusema hivyo vifaa walivyopewa vitasaidia sana kuchapisha nyaraka muhimu wakati wa utendaji.kulia ni Afisa Mtumishi Mkuu wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya,Bi. Aida Tesha.
Afisa Mtumishi Mkuu wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya,Bi. Aida Tesha (pili kushoto) akifungua moja ya box la kompyuta tayari kwa kukabidhi kwa Katibu Mtendaji wa Asasi ya Guluka Kwalala,Bw. Bernard Ndunguru (kushoto) ukiwa ni msaada uliotolewa na tume kwa Asasi hiyo.(pili kulia) ni Mkemia Mwandamizi wa wa Tume,Bw. Yovin Ivo na kulia kabisa ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Tume,Bi. Salome Mbonile.
Baadhi ya wanahabari wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mkemia Mwandamizi wa Tume,Bw. Yovin Ivo leo.

Kongamano la Viongozi Vitana wa Tanzania


Washiriki wa Kongamano la Viongozi Vijana wa Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 18 Septemba, 2010.


Wawakilishi wa Tanzania katika mkutano kati ya Rais Obama na viongozi vijana wa Afrika waandaa kongamano kwa viongozi vijana wa Tanzania

Hapo tarehe 18 Septemba wawakilishi watatu wa Tanzania katika mkutano kati ya Rais Barack Obama na Viongozi Vijana wa Afrika uliofanyika huko Washington DC kuanzia tarehe 3 hadi 5 Agosti 2010 waliandaa Kongamano kwa Viongozi Vijana wa Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Masoud Mohamed, Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana Zanzibar, Malula Nkanyemka, mshauri wa uendeshaji miradi mkoani Mwanza na Modesta Mahiga, Mkurugenzi Mtendaji wa Professional Approach Limited, Inc., waliwaalika vijana 50 kutoka mikoa yote ya Tanzania katika kongamano hilo lililojadili malengo ya Rais Obama kwa vijana wa Afrika.

Malengo hayo yanahimiza uwazi, uwajibikaji, jumuiya imara ya kiraia, kuendelezwa vijana katika ujasiriamali, matumizi ya teknolojia katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuongeza nafasi za ajira.

Bi. Mahiga alisema: "Leo ni mwanzo wa kile tunachotumaini kitakuwa kutaniko la kila robo mwaka la kikundi chetu kipya cha viongozi vijana. Tunataka kukuza elimu na kuchagiza kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yatakayowezesha kuongezeka kwa fursa za ajira kwa vijana.

Kwa kupitia michango yao kwa shughuli za kijamii, viongozi wa sekta binafsi wanaweza kuwainua na kuwajengea uwezo wanawake, watoto na vijana nchini Tanzania. Tutashirikiana nao, pamoja na wadau wengine katika kutekeleza malengo haya na kufikisha ujumbe kwa wawekezaji wa ndani na wa nje kwamba Tanzania ipo tayari na wazi kwa biashara."

Akitambua nguvu kubwa ya vijana katika bara hili kutokana na idadi na uwezo wao. Rais Obama alikutana na takriban viongozi vijana 115 kutoka katika mashirika na taasisi za kiraia na sekta binafsi kutoka katika zaidi ya nchi 40 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ili kukuza maendeleo na kujenga ubia na vijana wa Afrika.

Katika hotuba yake wakati wa Kongamano hilo, Afisa Uhusiano wa Umma wa Ubalozi wa Marekani, Bw. Ilya Levin aliwapongeza vijana hao kwa dira na uongozi wao katika kukabili changamoto zinazowakabili Watanzania hivi leo.

Aliwataka kutumia vyema fursa iliyopatikana kutokana na kongamano hili kupanua mtandao wao na kutumia uwezo mkubwa uliopo baina yao ili kuwezesha maendeleo makubwa zaidi.

"Kutokana na moyo mliouonyesha na kujitoa kwenu kikamilifu katika kutekeleza malengo yenu, kuna uwezekano mkubwa wa kupata msaada kutoka sekta binafsi na wadau wengine na hivyo kuwezesha mabadiliko ya kweli ambayo ndio kiu ya vijana wa Kitanzania hivi sasa,"alisema Levin.

Kongamano hili la viongozi vijana wa Kitanzania lilidhaminiwa na Watu wa Marekani kwa kupitia Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.

Sep 21, 2010

SERIKALI YASEMA HAKUTAKUWA NA MGAWO WA UMEME WAKATI WA UCHAGUZI!!

NA MAGRETH KINABO – MAELEZO

KAMPUNI ya Borodino kutoka nchini Urusi ya uwekezaji wa umeme imetia saini na Serikali ya Tanzania mkataba wa mradi wa umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji wenye uwezo wa kuzalisha 222 MV wenye thamani ya dola za Marekani milioni 700.

Makubaliano ya mkataba huo, yalitiwa saini jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya hiyo Razmik Tarverdyan katika ukumbi wa mkukutano wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Mradi huo unaojengwa katika eneo la Rumakali ,mkoani Iringa unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Akizungumzia kuhusu jijitahada za Serikali katika masuala ya umeme, Katibu Mkuu huyo, Jairo alisema wizara yake itahakikisha kuwa Tanzania haitarudi nyuma katika masuala ya nishati hiyo ili iweze kuwa chanzo kikuu cha usambazaji wa umeme kwa Afrika Mashariki na ya Kati.

“Tunataka tuondokane na mgawo wa umeme na kuwa na umeme wa kutosha ambao hutasafirishwa nchi za jirani,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo Jairo. Huku akiongeza kuwa hawatarajii kuwa na mgawo wa umeme wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Katibu Mkuu huyo alisema vyanzo vya umeme vitaendelezwa mfano vya maji ili kuifanya Tanzania iwe na umeme wa uhakika, tulivu na safi wenye bei nafuu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya hiyo Tarverdyan alisema mradi huo ni mkubwa katika uwekezaji wa nishati hiyo katika Afrika Mashariki, hivyo wamewekeza fedha hizo ili kubadilisha maisha ya Watanzania hususan walio kwenye eneo hilo .

Mahitaji halisi ya umeme nchini ni MW 897 wakati uzalishaji wa sasa ni zaidi ya MW 600.

DR. SALIM ASEMA NCHI BILA AMANI HAIWEZI KUFANYA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Mary Kweka, MAELEZO 21/09/2010

Amani ni msingi wa maendeleo na hivyo ni muhimu kwa nchi yoyote duniani kuhakikisha inalinda na kuidumisha ili iweze kufanya shughuli zake za maendeleo ,kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Dkt. Salim Ahmed Salim katika Siku ya Amani Duniani.

Dkt Salim, mwanadiplomasia mkongwe amesema kuwa bila amani nchi haiwezi kufanya shughuli za maendeleo na kuongeza kuwa hata pale ambapo maendeleo yameishapatikana huweza kuvurugwa endapo amani itatoweka katika nchi, ambapo mwaka huu kaulimbiu ni Wezesha Uwepo wa Amani.

Kwa nchi ambazo miaka ya hivi karibuni zimejitahidi kupiga hatua za maendeleo na zinaendelea kufanya jitihada kuhakikisha kuwa zinapiga hatua kubwa zaidi ya kudumisha amani ili kuleta maendeleo kwa faida ya wananchi wote”. Alifafanua Mh. Salim.

Amesema migogoro imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa shughuli za maendeleo sio tu kwa watu binafsi bali pia kwa taifa kwani nchi nyingi zenye migogoro Barani Afrika zimekuwa zikitumia fedha nyingi kusuluhisha migogoro na kununua silaha badala ya kuelekezwa kwenye huduma za kijamii kama Afya, Elimu ,Maji na zinginezo kuboresha maisha ya wananchi wao.

Matokeo ya migogoro yamesababisha hasara ya kiuchumi inayokadiriwa kuwa wastani wa Dola Bilon kumi na nane kwa kila mwaka kwa sababu ya migogoro na kulifanya Bara la Afrika kujulikana kama bara la mapigano jambo ambalo ni dhahiri linasikitisha.

Akitolea mfano wa nchi zenye migogoro ya muda mrefu kama Somalia, Dkt. Salim amesema ni changamoto kubwa kwa Bara hili na kwa jamii ya kimataifa kwa jumla na kwamba Afika haina budi kuendelea kufanya juhudi kwa kushirikiana na jumuiya ya kimatifa kupata ufumbuzi wa haraka.

Pia amevitaja vyanzo vya vya migogoro kuwa ni umaskini uliokithiri, ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, usambaratishaji wa demokrasia ,utumiaji wa siasa za ukabila na udini kwa maslahi ya muda mfupi ya wanasiasa na kutoheshimu matakwa ya watu wengi katika uchaguzi na kuwataka wanachi kuwa makini zaidi hasa kipindi hiki cha uchaguzi hapa nchini.

Aidha mwandiplomasia huyo amempongeza Dkt. Rais Jakaya Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika kumaliza migogoro mbalimbali, ikiwemo migogoro ya ndani kama ya nchi jirani Kenya

Maadhimisho ya siku ya Amani Duniani yamefanyika leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es salaam ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya mwaka wa Amani Barani Afrika kufuatia maamuzi yaliyotolewa na wakuu Nchi na Serikali za Wanachama wa Umoja wa Afrika 31 Agosti 2009.

FM ACADEMIA KUTAMBULISHA VUTA NIKUVUTE MBAGALA KUU!!

BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia Wazee wa
Ngweasuma' Ijumaa Septemba 24 watafanya utambulisho
maalum wa albamu yao mpya ya Vutanikuvute kwenye Ukumbi
wa Nawina Resort Mbagala Kuu.
Mratibu wa Onesho hilo Zahor Said, alisema kuwa usiku huo
maalum wa Ngwasuma utakuwa na burudani mbalimbali ambazo
zitausindikiza utambulisho huo.
Said alisema watafanya utambulisho huo kwa kusindikizwa na
vikundi vya unenguaji vya kiduku.
Alisema utambulisho huo wa albamu ya Vuta nikuvute utakuwa
chini ya Rais waNyoshi El Saadat watapiga nyimbo zote 11
zilizopo kwenye Albamu hiyo ikiwa ni pamoja na nyimbo za
zamani.
Nyimbo zilizobeba albamu hiyo kuwa ni Heshima kwa
Wanawake ambayo ilipata tunzo mwaka jana,Mwili wangu,
Usiku wa juma tano na Jasmini.
Nyimbo zingine ni Angalia shida yangu,Mgeni,Heiken
Ngwasuma,Moses Katumbi,Fadhila kwa mama Intro Ngwasuma
Mathematics na vuta ni kuvute ambayo imebeba jina la albam.
Usiku huo umedhaminiwa na Henkein Bear, Kampuni ya Inoch,
Blog za JaneJohn5, Mamapipiro na Full Shangwe.
Mwisho

Precision Air yazindua ndege yake ya saba mpya!

Precision Air -Shirika la ndege linaloongoza Tanzania, leo imezindua ndege yake ya saba mpya aina ya ATR 72-500 katika sherehe iliyofanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere-Terminal Two jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi wa ndege hiyo uliongozwa na Mwenyekiti wa IPP media Bw. Reginald Mengi kama mgeni rasmi na kuhudhuriwa pia na mabalozi, wadau wa biashara wa Precision Air pamoja na wafanyakazi wa shirika la ndege hilo.

Mkurugenzi Mkuu na Meneja

Mwendeshaji wa Precision Air, Bw. Alfonse Kioko alisema, “Mpango wetu wa kuongeza idadi za ndege ni mkakati madhubuti kabisa katika ukuaji wa kampuni na kutimiza huduma iliyo bora kwa wateja.”

Aliendelea: “Kutimia kwa ndege hizi mpya saba ni kuongezea nguvu ndege zetu tatu za zamani, kitu ambacho itatuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuweza kutimiza mahitaji ya wateja wetu kwa gharama nafuu zaidi. Hii ni kwa manufaa yetu sote, sisi na wateja wetu.”

Ndege hii mpya iliwasili tarehe 18 Septemba 2010 kutokea Toulouse-Ufaransa ambapo makao makuu ya ATR na kiwanda cha ndege kilipo. Ndege hizi aina ya ATR zimetengenezwa mahususi kabisa kwa namna ambayo madhara yake kwa mazingira na ya hali ya hewa ni mfinyu mno, kwa maana utoaji wake wa gesi aina ya kaboni ni mdogo. Hakika hii ni hatua na chaguo la kipekee kabisa kwa Precision Air kujali mazingira.

Ndege hiyo yenye usajili nambari 5H-PWG imepewa jina la Kilimanjaro, na imetengenezwa ikiwa na vifaa vya kisasa vya burudani kwa ajili ya wasafiri kuangalia sinema na kusikiliza muziki watakapokuwa wakisafiri. Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 66 tu ili iweze kutoa pia nafasi zaidi kwaajili ya mizigo ya abiria.

“Ndege hii imepewa jina la Kilimanjaro kwa sababu tofauti; Mosi, ni kwa heshima ya mchango mkubwa wa kibiashara ambao Precision inapata kutoka kwa watu wa Kilimanjaro, pili, kila sehemu ambayo ndege hii itakwenda, itatangaza kivutio cha utalii wa mlima mrefu kuliko yote Afrika, na ya mwisho, kama tu jinsi jina lake lilivyo, lengo letu ni kuwa shirika la ndege liliyojuu kuliko yote barani Afrika,” alisema Bw. Kioko.

Ridhiwani uso kwa uso na Chifu wa Wayao Tunduru!

Mlemavu wa viungo,Omar Chutira akitoa shukrani katika mkutano wa kampeni za kuhamasisha ushindi wa kishindo kwa CCM. katika Kata ya Namasakata, Tunduru,baada ya kupatiwa msaada wa sh. 160,000 za kununulia baiskeli ya magurudumu matatu zilizotolewa na Umoja wa Vijana wa CCM kwa maagizo ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Yusufu Makamba kufuatia ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Tunduru.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, Amoni Anastas akihutubia wakati wa mkutano wa kampeni za kuhamasisha ushindi kwa CCM juzi katika Kata ya Namasakata, Tunduru, mkoani Ruvuma.Amon ambaye ni mlemavu wa kuona, ana taaluma ya uanasheria.
Chifu Sultani Kalolo wa Kabila la Wayao, akijadiliana jambo na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Ridhiwani Kikwete katika makazi ya chifu huyo katika Kijiji cha Jakika, Tunduru, mkoani Ruvuma juzi. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)

Historia na utafiti kwa sanaa ya ubunifu ni muhimu kwa watanzania.

Imeelezwa kuwa ipo haja ya kufanyika utafiti wa kina na kuandika historia ya sanaa ya ubunifu wa mavazi hapa nchi, ili kuifahamisha jamii sanaa ya ubunifu ilikuwaje hapo nyuma, hivi sasa na mueleko wake wa baadae.

Ushauri huo umetolewa na mbunifu maarufu wa mavazi Tanzania Ndugu Mustafa Hassanali alipoluwa akiwasilisha mada ya hali ya sanaa ya ubunifu na changamoto wanazokabiliana nazo wasanii mbalimbali ambao wamejikita katika fani hiyo katika mkutano wa jukwaa la sanaa linalowakutanish wadau wa sanaa kutoka fani tofauti katika ukumbi wa BASATA, Ilala Sharifu Shamba jijini Dar es salaam.

“Ni vizuri tukajua kwa miaka iliyopita jamii ya watanzania walikuwa wakivaa mavazi ya aina gani? na kwa staili ipi?walikuwa wakifungaje vilemba, ni vazi la aina gani lilikuwa likipendwa zaidi, na mambo kama hayo ili kujua kama khanga, kitenge au vazi gani lilikuwa bora kwa wakati ule” Alisema Mustafa Hassanali.

Amesema BASATA iwapo itafanya hivyo itaisaidia jamii kupata taarifa hizo muhimu ambazo zitasaidia kujenga ufahamu wa kutosha wapi fani hii ilianzia, kwa sasa upo vipi na wasanii wafanye kuikuza na kunufaika nayo kama kazi nyingine.

Sambamba na hayo, aliishauri serikali kupitia wizara ya utamaduni na michezo, kuandaa sera ya sanaa ya ubunifu wa mavazi itakayosaidia kutoa muongozo katika sekta hiyo na ya sanaa ya ubunifu ambayo inakuwa siku hadi siku hapa nchini.

Hassanali amesema sambamba na sekta hiyo kukua bado haijatoa ajira tosha kwa wasanii kwani haijafikia uwezo wa kuuza na kufikiwa kwa malengo ya wasanii ambao siku zote wamekuwa mstari wa mbele katika ubunifu.

Aidha Mustafa amesema kuwa itakuwa ni jambo la busara iwapo itaandaliwa siku maalumu ya sanaa hapa nchini, siku itakayoakutanisha wasanii wa fani mbalimbali na kukaa pamoja kuweza kuangalia wapi wametoka, walipo na changamoto mbalimbali zinazowakabli na jinsi ya kukabiliana nazo.

“Siku zote umoja ni nguvu, na itapendeza iwapo wasanii watakutana pamo

ja na kupata fursa ya kujadili na kuzungumza mambo mbalimbali, pamoja na kuibua mbinu mpya za kuleta mafanikio katika fani ya sanaa hapa nchini.

Aidha mbunifu huyo wa mavazi aliongeza kuwa wasanii wa fani ya ubunifu wa mavazi wapatiwe fursa za kushiriki katika matukio mbailimbali yanayoandaliwa na serikali na taasisi mbalimbali kwani wanaowezo wa kutoa mchango mkubwa kufanikisha matukio hayo kupitia kazi zao.

MAKAMU WA RAIS WA SHIRIKA LA HABARI LA XINHUA -CHINA ATEMBELEA TANZANIA.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Clement Mshana (kushoto) akiwa ameongozana na Makamu wa Rais wa Shirika la Habari la Xinhua - China Mr. Liu Yue mara baada ya kumpokea jana usiku katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.Katikati ni Mwakilishi wa shirika hilo nchini Tanzania Bi. Guo Chunju.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Clement Mshana akiwa katika mazungumzo mfupi na Makamu wa Rais wa Shirika la Habari la la Xinhua - China Mr. Liu Yue jana usiku jijini Dar es salaam mara baada ya kumpokea. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Raphael Hokororo, Mshauri wa masuala ya siasa wa ubalozi wa China- Tanzania Mr. Fu Jiqun na Mwakilishi wa shirika Xinhua nchini Tanzania Bi. Guo Chunju.Picha na Aron Msigwa

MAMA SALMA KIKWETE AKIWA KOROGWE!!

Wagombea Ubunge kutoka jimbo la Korogwe Mjini Mkoani Tanga Yussuph Nassir (kulia) na Mgombea wa Jimbo la Korogwe vijijiniProf. Ngonyani Majimarefu wakitambulishwa kwa wanachama wa UWT 20-9-2010 katika mkutano wa ndani wa wanachama wa UWT anmapo Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete amezungumza nao kuhusu umuhimu wa kuja kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu ifikapo Oktoba 31 mwaka huu.Picha na Mwanakombo Jumaa.
Mama Salma Kikwete akiongea na wanachama wa UWT wa Wilaya ya Tanga mjini
Baadhi ya wagombe Udiwani kupitia CCM Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga wakitambulishwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake (WAMA) Mama Salma Kikwete 20-9-2010 katika mkutano wa ndani wakuongea na wanachama wa UWT wa wilaya hiyo kuhusu umuhimu wa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 31,mwaka huu. Picha na Mwanakombo Jumaa
mtu na Mke wake walikuwa wanachama wa CUF lakini wamekihama chama cha CUF na kujiunga na CCM huko Kabuku Wilaya ya Handeni Mkaoni Tanga.

wamiliki wa kumbi watakiwa kusajili kumbi zao BASATA


Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego akisisitiza jambo.Alisema kwamba,BASATA linatoa muda hadi Desemba mwaka huu wamiliki wote wa kumbi wawe wamesajili kumbi zao vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi,Mzee Nkwama Bhalanga alipendekeza kwamba, waandaaji wa matukio ya sanaa wawe wanapewa masharti magumu yakiwemo ya kutaja idadi ya watu wanaohudhuria kwenye onyesho lao na sifa za ukumbi.
Mbunifu wa mavazi maarufu nchini,Mustapha Hassanally naye aliwasilisha mada yake kuhusu Soko la Sanaa ya Ubunifu wa Mavazi Tanzania na Changamoto zinazowakabili.



********** ******** ***********

Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imetoa miezi mitatu hadi Desemba 31 mwaka huu kwa wamiliki wa kumbi kuhakikisha wanafuata kanuni, taratibu na sheria za kuendesha kumbi zao ikiwa ni pamoja na kuzisajili Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.


Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu BASATA, Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Bw.Seth Kamuhanda alisema kwamba, kumekuwa na ukiukwaji wa makusudi wa sheria,kanuni na taratibu za kuendesha kumbi hali ambayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa yakiwemo yale yaliyotokea Tabora mwaka jana na yale ya Sherehe za Idd El Fetri kwenye Ukumbi wa Luxury wilayani Temeke,Dar es Salaam.


“Tatizo kubwa la watanzania, ni kufanya mambo kiholela, kutokufuata sheria, kanuni na taratibu.Hili limekuwa kwenye mazoea na kwa kiasi kikubwa limekuwa likisababisha matatizo mengi yakiwemo majanga kama yale ya Tabora na Temeke kwenye Ukumbi wa Luxury” alisema.


Alisisitiza kwamba, serikali kamwe haiwezi kuendelea kufumbia macho vitendo visivyozingatia sheria hivyo wamiliki wa kumbi lazima wahakikishe wanafanya marekebisho kwenye kumbi zao na kuhakikisha kufikia Desemba mwaka huu zinakuwa ziko kwenye kiwango kinachokubalika kisheria na zimesajiliwa Baraza la Sanaa la Taifa.


“Serikali inasikitishwa sana na vifo ambavyo vimekuwa vikitokea kwenye kumbi za burudani hasa vya watoto na vijana na inaagiza wadau wote wa burudani hasa wamiliki wa kumbi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo zinazosimamiwa na BASATA”, aliongeza.


Awali Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alizitaja sifa za kumbi zinazokubalika kisheria kuwa ni pamoja na kuwa na milango ya kutosha inayofungukia nje,vyoo nadhifu vya wanawake na wanaume, miundombinu kwa walemavu, vifaa vya kuzimia moto, maegesho ya vyombo vya usafiri na ulinzi kamili.


Aidha, alisema kuwa kumbi zote lazima zisajiliwe Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lakini changamoto kubwa ni kasi ndogo ya wamiliki kusajili kumbi zao.Katika hili Katibu Mkuu,Bw.Kamuhanda alisema kwamba, ifikapo Desemba mwaka huu kama kutakuwa na kumbi zitakuwa hazijasajiliwa basi hatua kali za kisheria zichukuliwe.


Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Bw.Profesa Hermas Mwansoko alisisitiza kwamba, muda uliotolewa kwa wamiliki wa kumbi kurekebisha kumbi zao ili ziendeshwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ni wa mwisho na baada ya hapo hakutakuwa na huruma yoyote.


“Nafasi hii ni ya mwisho kwa wamiliki wa kumbi,BASATA wameshatoa maelekezo yote kuhusu sifa za kumbi.Hatutakuja kukumbushana tena suala hili lazima wamiliki wa kumbi watumie fursa hii iliyotolewa na serikali kufanya marekebisho” aliongeza Profesa Mwansoko.


Pamoja na Jukwaa la Sanaa wiki hii kujikita kwenye suala la kumbi masuala mbalimbali yaliibuka ikiwemo mada ya Soko la Sanaa ya Ubunifu wa Mavazi Tanzania na Changamoto zinazowakabili iliyowasilishwa na mbunifu maarufu wa mavazi Mustapha Hassanaly na kuvuta hisia za wadau wengi.


Wiki ijayo katika Jukwaa la Sanaa, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT) Bw.Kajubi Mkajanga atazungumzia mada ya Vyombo vya Habari na Utandawazi Katika Tasnia ya Sanaa.

Sep 20, 2010

TIMU YA KINONDONI YANYAKUWA UBINGWA WA POOL BAADA YA KUICHAPA TEMEKE!!

Timu ya mkoa wa kinondoni baada ya kutoa ubingwa wakiwa wamenyakua kombe kwa furaha kabisa na ubingwa huo umetokana na kuifunga temeke magoli 15 kwa 10 . Timu ya Kinondoni imenyakua ubingwa wa taifa wa mashindano ya pool baada ya kuifunga Temeke huku mchezaji wa kike Viorety Mrema akitokea Kinondoni akinyakua ubingwa huo na kujishindia tiketi ya kwenda nchini ufaransa mwaka huu kushiriki mashindano ya dunia. Katika mashindano hayo pia mchezaji BONIFACE JOHN kutoka Arusha amenyakua ubingwa kwa upande wa wanaume na kufanikiwa kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Pool itakayokwenda nchini Ufaransa Picha kwa hisani ya www.Janejohn5.blog

TPDF na makakati wa kuboresha huduma zake!!

Mwandishi Wetu, JESHI la Wananchi Tanzania (TPDF) limesema litaendelea kushirikiana na kampuni, watu binafsi na mashirika mbalimbali katika kuhakikisha linaboresha huduma za kijamii kwa wanajeshi na familia zao. Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki Mkuu wa Kitengo cha Maduka, Vinywaji na Mikopo jeshini Meja C.J Kapandamtava alisema hatua hiyo pamoja na kujenga mahusiano na jamii ya kitanzania lakini pia itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wanajeshi wake kupata huduma wanazozitaka kwa wakati kulingana na mahitaji. Meja Kapandamtava aliyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kinywaji kipya cha bia ya Kopo ya Heineken 25cl ‘Heineken Balozi ‘ maalumu kwa matumizi ya Jeshi iliyofanyika katika ukumbi wa jeshi wa kambi ya Lugalo Dar es Salaam. Alisema huduma za kijamii zinazopatikana katika maeneo ya makambi ikiwemo vinywaji vya aina mbalimbali havilengi kupata faida na kwamba hatua hiyo ni maalumu kwa wanajeshi kutokana na majukumu ya kitaifa waliyonayo. “Kuzinduliwa kwa kinywaji hiki jeshini kutatufanya tuendelee kuboresha wigo wa upatikanaji wa huduma za kijamii na kama tunavyojua sisi huku kwetu tunatoa huduma zaidi kuliko kulenga faida ikiwa ni utaratibu maalumu kwa jeshi kutokana na majukumu yao kitaifa,’ alisema. Aliwaasa wanajeshi kuitumia huduma hiyo kama ilivyolengwa na kuhakikisha kuwa vinywaji hivyo havipelekwi kwenye maduka uraiani. Kwa upande wake Kanali Harry Andrew Msechu aliyekuwa mgeni rasmi alisema jeshi kama mhimili mmojawapo wa taifa linapaswa kuangaliwa na kupewa huduma zenye ubora wa kimataifa kama kilivyo kinywaji hicho kinachotumiwa na nchi nyingi duniani. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mabibo Benedicta Rugemalira alisema ingawa bia ya Heineken tayari ilikuwepo jeshini katika ujazo wa 33cl bado wameona kuna umuhimu wa kupanua wigo wa kupatikana kwa kinywjai hicho hususani kwa kuzingatia bei. Alisema Heineken 33cl ya chupa yenye shingo fupi kwa kipindi kirefu imekuwa ikitumika jeshini na kuuzwa kwa sh. 1,300/- na kwamba kinywaji hicho kipya cha kopo katika ujazo wa 25cl kimeingizwa jeshini na kitauza kwa sh. 1,000/-. Alisema hatua hiyo ni katika kuwajali wanajeshi kutokana na majukumu mazito waliyonayo katika ujenzi wa taifa na kwamba hiyo ni sehemu ya uwajibikaji wa kampuni hiyo kwa jamii ya kitanzania kulingana na majukumu yanayowakabili. Rugemalira aliongeza kwa kushukuru uongozi wa Makao Makuu ya Jeshi hususani upande wa vinywaji kutokana na ushirikiano mkubwa wanaoupata na kwamba kampuni hiyo itahakikisha mahusiano hayo yanaendelea kudumishwa kadri siku zinavyoendelea. “Tayari tulikuwa na Heineken jeshini lakini kwa ujazo wa 33cl inayouzwa sh. 1,300/- na kwamba bei hii wakati fulani ilikuwa inawanyima haki wale waliokuwa na uwezo mdogo hivyo tumeona tupeleke kinywaji kingine kwa bei ambayo wengi wataimudu,tunawashukuru jeshi kwa ushirikiano wanaotupa,” alisema Rugemalira.

THE DON HIMSELF

Karibuni sana kwenye blog hii ya kijamii iliyosheheni makila kitu kuanzia siasa uchumi afya na burudani kwa ujumla wake.uingiapo kwenye blog hii ni mengi ambayo utapata nafasi ya kukutana nayo,kumbuka mawazo yako ndo hasa yanayojenga na kunifanya niwe na ufanisi zaidi.kariiiiiiibuuuuuuuuuuuu saaaaaaaaaaaaaaanaaaaaaaaaa.(THE DJ HIMSELF-JIWE)

Followers

BLOG ZA MARAFIKI

Search This Blog

ZILIZOPITA

DUNIA MUZIMA