Asasi ya Agenda Participation 2000 asasi isiyo ya kiserikali inayofanya kazi ya kuhamasisha utamaduni wa utawala bora na demokrasia ndani ya Tanzania. Asasi pamoja na mambo mengine inatoa elimu ya uraia, mafunzo na kuhifadhi masuala ambayo yanaweza kuimarisha ushiriki wa wananchi katika utawala, demokrasia na michakato ya maendeleo.
AP2000, ikiongozwa na Dira ya; “Kuona jamii ya kidemokrasia na yenye amani na dola au nchi inayoendeshwa na utamaduni wa misingi au kanuni za kidemokrasia”. AP2000 imekuwa ikiratibu tangu mwaka 2005 na pia mwaka huu 2010 mchakato wa kukusanya na kuboresha maoni ya wanaharakati wasio wa kiserikali katika masuala mbali mbali nyeti kwa maslahi ya Taifa letu.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, AP2000 imehusika kuratibu uandaaji wa Tamko la Wanaharakati Wasio wa Kiserikali kwa msaada wa mashirika mbalimbali kwa taarifa na ushauri. Sambamba na mashirika hayo, kwa namna ya pekee Shirika la Kijerumani la Friedrich Ebert Stiftung, wamehusika kufadhili uchapaji, uzinduzi na usambazaji wa tamko hili.
Tamko la Wanaharakati Wasio wa Kiserikali tunalolizindua leo kupitia mgeni rasmi Mhe. Jaji Mstaafu Lameck Mfalila, 21.09.2010 katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar-es-Salaam likishuhudiwa na wanaharakati toka Asasi za kiraia, Balozi, Mashirika ya Kimataifa, Wanahabari, na wananchi wote kwa ujumla toka kila pembe ya Tanzania limegusa maeneo makuu yafuatayo;
- Tathmini ya Maendeleo Kiuchumu na Haki
- Ajira
- Mazingira na Maliasili
- Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
- Huduma za Jamii
- Uongozi na Utawala
- Rushwa
- Maisha na Usalama wa Binadamu
- Maadili ya Uchaguzi
Vipaumbele hivi vilivyofafanuliwa kwa kina sana katika chapisho la Tamko hili, vinaangaliwa na Wanaharakati Wasio Wakiserikali kama msingi wa kupiga kura wagombea kutoka vyama vya siasa. Sambamba, kuwataka wagombea ngazi za Udiwani, Ubunge na Urais pia viongozi na watumishi wa umma kuzingatia maazimio hayo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2010.
Maazimio haya yanabeba uzito na masuala nyeti yanayoikandamiza Taifa na kuzidi kuliweka katika hali ngumu na kikwazo kuelekea ustawi na maendeleo endapo hayatashughulikiwa kwa haraka na kiukamilifu
Uchaguzi Mkuu unatoa nafasi adhimu kwa wapiga kura na wagombea kukumbuka malengo ya msingi ya mfumo wa uchaguzi, yaani kuweka mbele na kulinda maslahi ya Taifa hili. Kwa mantiki hiyo, tunasisitiza uwepo wa mchakato wa uchaguzi wenye uwazi, haki na amani.Lakini pia, tunapinga vikali aina yoyote ya vitisho, rushwa, mizengwe au hila kupindisha ushindi utokanao na kura halali za wananchi.Tunasisitiza katika siasa safi zenye kuzingatia misingi ya kidemokrasia.
Haya ndiyo tunayoyaamini, tunayoyasimamia, tuna amini yana msingi sasa na hata baada ya Uchaguzi Mkuu 2010. Wagombea watakaoingia madarakani, viongozi wa umma wote wanapaswa kuyasimamia kwa vitendo kwa maslahi na ustawi wa Taifa letu.
Tanzania tunayotaka kuiona ni Taifa lenye amani na maendeleo ambalo linaheshimu haki za wananchi
wake wote bila kujali jinsia, hadhi, dini, kabila, imani ya kundi fulani na uwezo kimwili ama kiuchumi. Tunataka Tanzania ambayo licha ya kutokuwa na wala rushwa, inaendeshwa na viongozi wenye uvumilivu na uadilifu, wenye kutumia ipasavyo maliasili na rasilimali hususan watu. Tunataka Tanzania inayojitosheleza kwa chakula; yenye miundombinu bora yenye misingi ya kiteknolojia; na yenye kutafsiri maendeleo ya kitaifa kwa kuangalia afya, elimu na ustawi wa jamii. Tunaomba wananchi wote wayasimamie haya na kuyafatilia, kwa sababu Tanzania tunayotaka inawezekana.
Ninawashukuru sana kwa kufika kwenu katika uzinduzi huu. Ni matumaini yangu makubwa mtaupasha umma vizuri juu ya haya tuliyowasilisha kwa umma kupitia tamko hili.
Mungu Ibariki Tanzania!
Imetolewa na;
Mwenyekiti, Agenda Participation 2000.
No comments:
Post a Comment