Sep 22, 2010

Buriani Dk. Ernest Mashimba!!

Na Barnabas Lugwisha

Jumapili usiku, mida ya saa mbili hivi Mwandishi mwenzangu wa Habari , Mbaraka Islam, alinipigia simu na kuniuliza, “kaka umesikia kwamba Dk.Mashimba amefariki,” nikamwabia sijui kwa kweli, akasema hebu fuatilia, nikawapigia simu Wahariri watatu Absolom Kibanda, John Mapinduzi na Jackson Manyerere nikapata hakikisho.

Ni kweli ametutoka msomi huyu na kazi ya Mungu haina makosa, alikuwa mtu asiye na majivuno, mpenda utani na pande la baba kama ilivyo kwa wanaume wengi wa kisukuma.

Kabla ya umauti kumfika, alinusurika kifo mwanzoni mwa miaka ya 2000 maeneo ya Chango’mbe ambapo dereva wake alifariki hapo hapo, ilikuwa ni ajali ya kugongana na nadhani na daladala.

Alitibiwa na akapona, alivyokuwa muhimbili amelezwa alipata fahamu na kuagiza wasaidizi wake wanipe maelekezo kwamba niandike stori ambayo itaonyesha kwamba anaendelea pia nilizungumza naye kwa simu na akaniambia “Lugwisha, waambie wananchi sijafa, niko hai, kaandike hivyo poti,” kweli nikaandika hivyo akafurahi sana, baadaye alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na akapona.

Dk. Mashimba hakuwa na mbwembe kama ilivyo kwa wasomi wengi wa ngazi yake, ambao wengi wao huwa na mikogo na kujifanya Miungu watu kana kwamba hawatauonja umauti.

We fikiria wakati mwingine nilikuwa nakunywa naye supu ya utumbo pale Chuo Cha Usimamisi wa Fedha (IFM), nani mwenye nafasi kama yake atafanya hivyo, wengi hujiona miungu watu, kwa Dk Mashimba haikuwa hivyo na simpambi kwa kuwa ametangulia mbele ya haki, alikuwa ni mtu wa watu ,ni nadra sana kumuona amevaa suti, labda kuwe na ugeni mzito kwake.

Mwaka 2005 niliandika makala yake moja yenye kichwa “Mkemia Mkuu Asiyevaa” suti, nilidhani atakasirika lakini, kumbe alifurahi sana , akaikata ile makala na kuibandika kwenye ubao wa matangazo pale nje ya ofisi yake.

Nilifahamiana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1997 nikiwa Mwandishi wa The African maeneo ya Idara ya Habari Maelezo nakutana, nakumbuka ilikuwa ni kwenye mkutano wa Waandishi wa Habari, wakati huo Dr Mashimba alikuwa ameambatana na Waziri wa Afya wa wakati huo, Dr Aron Chiduo.

Ndani ya Mkutano huo nilimbana bana na maswali Dr Mashimba ambaye alikuwa akimsaidia Dk Chuduo kutoa ufafanuzi masuala mbalimbali.

Tulipomaliza Mkutano huo Dr Mashimba alinialika Ofisini kwake pale jirani na Hospitali ya Ocean Road na kuanza kufahamiana naye na kasha nikawa nafanya kazi za Uhusiano wa Umma za Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa takriban miaka saba hivi.

Kilichonivutia katika historia ya Dk Mashimba ambaye leo hatunaye ni historia ya maisha yake , ni Msukuma wa Ngudu, Kwimba lakini amesomea Zanzibar kuanzia Darasa la kwanza hadi alipojiunga na chuo kikuu Cha Dar es Salaam mwazoni mwa miaka 1980, kabla serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijampeleka nchini Australia kwa masomo ya ya shahada ya Pili na shahada ya Uzamivu (PHD).

Alivyorudi nchini kutoka ughaibuni mwaka 1995 , alipandishiwa cheo na kuwa Mkemia Mkuu wa Zanzibar, japo alikuwa amekaa Zanzibar tangu utoto wake lafudhi yake haikubadilika, ilikuwa ni ya Kisukuma tu, mwaka 1996 iliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuwa Mkemia Mkuu wa Zanzibar alikuwa akiendesha daladala, nilimuuliza kuhusu ukweli huo alikubali.

“Ndiyo poti kwani nikiendesha daladala kuna nini, si ya kwangu bwana”, alisema huku akicheka.

Tukiaachana na hayo, atakumbukwa kwa kufanya mambo mengi pale Maabara ya Mkemia Mkuu, chini ya utawala wake, maabara iliboreshwa, aliwezesha mashine ya DNA kununuliwa na alijenga Maabara ya Kanda pale Mwanza.Alikuwa ni mchapa kazi kwelikweli.

Alitupeleka kozi mbalimbali baadhi ya Waandishi wa Habari zihusuzo maswala ya Maabara yake na kwa kweli huduma mbalimbali ziliboreshwa na kuuzingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao kwake yeye ndiyo ilikuwa ilani ya utendaji wake.

Aliiboresha Maabara kwa vifaa mbalimbali vya kisasa muda mwingi alikuwa akiwahurumia wachimbaji madini wadogo wadogo wanaotumia madini ya Mercury kusafishia madini yao .

Alianzisha huduma za elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa kupima maji ya visima kwenye maabara yake kwali aliamini kwamba visima vingi vya maji ya kunywa hapa jijini si salama,.

Nilimshawishi kuanzisha jarida la Elimu ya Ukemia kwa Umma, alikubali na nikapata bahati ya kuwa muhariri wa kwanza jarida hilo , kwa kufanya kazi kwa karibu na Dk.Mashimba nilipata nafasi ya kujifunza mambo mengi ya yahusiyo tasnia hiyo muhimu ya Ukemia hapa nchini.

Nakumbuka kuna wakati ilitokea mvutano baina ya serikali ya mapinduzi Zanzibar na Muungano, Zanzibar walitaka akafanye kazi kwao kwa kuzingatia kwamba serikali ya mapinduzi ndiyo iliyomsomesha.

Amefariki akiwa usingizini, ilikuwa ni mipango ya Mungu, ametangulia na sisi tuko nyuma yake.

Ulale Mahale pema peponi Dk. Mashimba.

No comments:

THE DON HIMSELF

Karibuni sana kwenye blog hii ya kijamii iliyosheheni makila kitu kuanzia siasa uchumi afya na burudani kwa ujumla wake.uingiapo kwenye blog hii ni mengi ambayo utapata nafasi ya kukutana nayo,kumbuka mawazo yako ndo hasa yanayojenga na kunifanya niwe na ufanisi zaidi.kariiiiiiibuuuuuuuuuuuu saaaaaaaaaaaaaaanaaaaaaaaaa.(THE DJ HIMSELF-JIWE)

Followers

BLOG ZA MARAFIKI

Search This Blog

ZILIZOPITA

DUNIA MUZIMA