Washiriki wa Kongamano la Viongozi Vijana wa Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 18 Septemba, 2010.
Wawakilishi wa Tanzania katika mkutano kati ya Rais Obama na viongozi vijana wa Afrika waandaa kongamano kwa viongozi vijana wa Tanzania
Hapo tarehe 18 Septemba wawakilishi watatu wa Tanzania katika mkutano kati ya Rais Barack Obama na Viongozi Vijana wa Afrika uliofanyika huko Washington DC kuanzia tarehe 3 hadi 5 Agosti 2010 waliandaa Kongamano kwa Viongozi Vijana wa Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Dar es Salaam.
Masoud Mohamed, Mwenyekiti wa Mtandao wa Vijana Zanzibar, Malula Nkanyemka, mshauri wa uendeshaji miradi mkoani Mwanza na Modesta Mahiga, Mkurugenzi Mtendaji wa Professional Approach Limited, Inc., waliwaalika vijana 50 kutoka mikoa yote ya Tanzania katika kongamano hilo lililojadili malengo ya Rais Obama kwa vijana wa Afrika.
Malengo hayo yanahimiza uwazi, uwajibikaji, jumuiya imara ya kiraia, kuendelezwa vijana katika ujasiriamali, matumizi ya teknolojia katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuongeza nafasi za ajira.
Bi. Mahiga alisema: "Leo ni mwanzo wa kile tunachotumaini kitakuwa kutaniko la kila robo mwaka la kikundi chetu kipya cha viongozi vijana. Tunataka kukuza elimu na kuchagiza kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yatakayowezesha kuongezeka kwa fursa za ajira kwa vijana.
Kwa kupitia michango yao kwa shughuli za kijamii, viongozi wa sekta binafsi wanaweza kuwainua na kuwajengea uwezo wanawake, watoto na vijana nchini Tanzania. Tutashirikiana nao, pamoja na wadau wengine katika kutekeleza malengo haya na kufikisha ujumbe kwa wawekezaji wa ndani na wa nje kwamba Tanzania ipo tayari na wazi kwa biashara."
Akitambua nguvu kubwa ya vijana katika bara hili kutokana na idadi na uwezo wao. Rais Obama alikutana na takriban viongozi vijana 115 kutoka katika mashirika na taasisi za kiraia na sekta binafsi kutoka katika zaidi ya nchi 40 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ili kukuza maendeleo na kujenga ubia na vijana wa Afrika.
Katika hotuba yake wakati wa Kongamano hilo, Afisa Uhusiano wa Umma wa Ubalozi wa Marekani, Bw. Ilya Levin aliwapongeza vijana hao kwa dira na uongozi wao katika kukabili changamoto zinazowakabili Watanzania hivi leo.
Aliwataka kutumia vyema fursa iliyopatikana kutokana na kongamano hili kupanua mtandao wao na kutumia uwezo mkubwa uliopo baina yao ili kuwezesha maendeleo makubwa zaidi.
"Kutokana na moyo mliouonyesha na kujitoa kwenu kikamilifu katika kutekeleza malengo yenu, kuna uwezekano mkubwa wa kupata msaada kutoka sekta binafsi na wadau wengine na hivyo kuwezesha mabadiliko ya kweli ambayo ndio kiu ya vijana wa Kitanzania hivi sasa,"alisema Levin.
Kongamano hili la viongozi vijana wa Kitanzania lilidhaminiwa na Watu wa Marekani kwa kupitia Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment