
Mary Kweka, MAELEZO 21/09/2010
Amani ni msingi wa maendeleo na hivyo ni muhimu kwa nchi yoyote duniani kuhakikisha inalinda na kuidumisha ili iweze kufanya shughuli zake za maendeleo ,kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Dkt. Salim Ahmed Salim katika Siku ya Amani Duniani.
Dkt Salim, mwanadiplomasia mkongwe amesema kuwa bila amani nchi haiwezi kufanya shughuli za maendeleo na kuongeza kuwa hata pale ambapo maendeleo yameishapatikana huweza kuvurugwa endapo amani itatoweka katika nchi, ambapo mwaka huu kaulimbiu ni Wezesha Uwepo wa Amani.
“ Kwa nchi ambazo miaka ya hivi karibuni zimejitahidi kupiga hatua za maendeleo na zinaendelea kufanya jitihada kuhakikisha kuwa zinapiga hatua kubwa zaidi ya kudumisha amani ili kuleta maendeleo kwa faida ya wananchi wote”. Alifafanua Mh. Salim.
Amesema migogoro imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa shughuli za maendeleo sio tu kwa watu binafsi bali pia kwa taifa kwani nchi nyingi zenye migogoro Barani Afrika zimekuwa zikitumia fedha nyingi kusuluhisha migogoro na kununua silaha badala ya kuelekezwa kwenye huduma za kijamii kama Afya, Elimu ,Maji na zinginezo kuboresha maisha ya wananchi wao.
Matokeo ya migogoro yamesababisha hasara ya kiuchumi inayokadiriwa kuwa wastani wa Dola Bilon kumi na nane kwa kila mwaka kwa sababu ya migogoro na kulifanya Bara la Afrika kujulikana kama bara la mapigano jambo ambalo ni dhahiri linasikitisha.
Akitolea mfano wa nchi zenye migogoro ya muda mrefu kama Somalia, Dkt. Salim amesema ni changamoto kubwa kwa Bara hili na kwa jamii ya kimataifa kwa jumla na kwamba Afika haina budi kuendelea kufanya juhudi kwa kushirikiana na jumuiya ya kimatifa kupata ufumbuzi wa haraka.
Pia amevitaja vyanzo vya vya migogoro kuwa ni umaskini uliokithiri, ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, usambaratishaji wa demokrasia ,utumiaji wa siasa za ukabila na udini kwa maslahi ya muda mfupi ya wanasiasa na kutoheshimu matakwa ya watu wengi katika uchaguzi na kuwataka wanachi kuwa makini zaidi hasa kipindi hiki cha uchaguzi hapa nchini.
Aidha mwandiplomasia huyo amempongeza Dkt. Rais Jakaya Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika kumaliza migogoro mbalimbali, ikiwemo migogoro ya ndani kama ya nchi jirani Kenya
Maadhimisho ya siku ya Amani Duniani yamefanyika leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es salaam ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya mwaka wa Amani Barani Afrika kufuatia maamuzi yaliyotolewa na wakuu Nchi na Serikali za Wanachama wa Umoja wa Afrika 31 Agosti 2009.
No comments:
Post a Comment