


Ni globu ya kijamii inayojihusisha na mambo yote ya kijamii,natumaini jamii yangu ya kitanzania itafaidika sana pindi ichukuapo fursa ya kuperuzi kwenye globu hii,dhamira yangu ni kufikisha ujumbe pamoja na kuiburudisha jamii yangu na furaha yangu ni kuona natimiza dhamira yangu kwako.natumaini kuwa wewe utaniunga mkono kwa kile ambacho nataka kukifanya kwa ajili ya jamii yangu ya kitanzania.NASHUKURU KWA KUNIELEWA.
Washiriki wa mashindano ya kuvua samaki ya Vodacom Lathan Open 2010 waliokuwa wakiendesha boti ya Natasha wakishangilia kwa kunyoosha vidole vyao juu mara baada ya kukabidhiwa zawadi zao za ushindi wa kuvua samaki wengi zaidi, mashindano hayo yamefanyika jana kwenye kisiwa cha Sinde kwenye Bahari ya Hindi, kushoto ni Necta Foya Meneja wa Mawasiliano Vodacom
Bw. David Sutton wa boti ya uvuvi ya Simba kulia akionyesha zawadi yake aliyoipokea kutoka kwa Mkuu wa Udhamini wa Vodacom Tanzania George Rwehumbiza mara baada ya boti yao kuwa miongoni mwa washindi wa jumla walioshinda kuvua samaki wengi zaidi katika mashindano ya Vodacom Lathan Open 2010 yaliyofanyika kwenye kisiwa cha Sinda jana, kushoto ni Necta Foya Meneja wa Mawasiliano Vodacom Tanzania.
Na. Mary Kweka – MAELEZO.
Dar es Salaam.
Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora imesema itaendelea kulinda, kutetea , na kushughulikia malalamiko mbalimbali ya uvunjwaji wa Haki za binadamu kwa watoto nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Kiongozi Mstaafu Ramadhani Manento wakati akizungumza na viongozi wa mabaraza ya watoto waliofanya ziara ofisi kwake ikiwa ni sehemu ya kongamano lao la mwaka huu linalomalizika leo ( jumamosi) jijini Dar es salaam.
Alisema ili kujenga taifa bora lenye maadili , jamii inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa na kuthaminiwa pamoja na kupatiwa mahitaji mbalimbali yakiwemo Elimu, Malazi bora, haki ya kupendwa, uhuru wa kucheza na kutoa maoni.
Aliongeza kuwa katika kulinda na kutetea haki za watoto, Serikali kupitia tume ya haki za binadamu na Utawala Bora imeanzisha Dawati la watoto ambalo linawajibika na kupokea malalamiko mbalimbali ya uvunjwaji wa haki za biadamu kwa watoto.
“Dawati la watoto linawajibika kulinda na kutetea haki za watoto wanaoishi katika mazingira magumu, walioachishwa shule,matatizo ya miradhi, utekelezaji wa sheria ya ubakaji wa watoto kwa watuhumiwa na mazingira ya watoto walio magerezani “Alifafanua Jaji Manento.
Aliendelea kufafanua kuwa Dawati hilo linatoa elimu kwa watu hasa wazazi kutambua umuhimu wa haki za watoto na kuwa makini pale wanapotoa adhabu kwa watoto huku akitoa angalizo kwa wazazi kuwa makini na adhabu hizo kuwa ziwe na vikomo na si zakuwajeruhi watoto na kuwasababishia ulemavu na kuwapotezea maisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti na Nyaraka wa tume hiyo Bi Epifania Mfundo alisema mwaka huu dawati la watoto limepokea jumla ya malalamiko 114 mpaka sasa, na wamefanikiwa kushughulikia malalamiko 28 kati ya 114 yaliyowasilishwa kwenye tume ya haki za binadamu na utawala bora.
Benjamin Sawe
Maelezo
Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua ndugu Nape Moses Nnauye kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.
Bwana Nnauye amechukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Said Ali Amanzi ambaye amebadilishiwa kituo chake cha kazi na kuhamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Kabla ya uteuzi huo Ndugu Nnauye alikuwa ni Katibu Msaidizi Idara ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa CCM Makuu Dar es Salaam wakati Bwana Said Ali Amanzi amechukua nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Ndugu Cleopas Rugarabamu ambaye alifariki mwezi Julai mwaka huu akiwa kwenye matibabu nchini India.
NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
SERIKALI imetoa sh. bilioni 23.8 kwa ajili ya kununua mahindi tani 200,000 kutoka kwa wakulima wa ili kuweza kuyahifadhi katika Hifadhi ya Taifa kwa ajili ya matumizi ya baadae, vikiwemo vifaa vingine kama vile ni mizani , dawa za kufukuzia wadudu na mashine.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira jijini Da res Salaam jana(leo) ambapo alisema Rais Jakaya Kikwete ameagiza tani 400, 000 za mahindi zinunuliwe ikiwa ni lengo la Serikali katika kuyahifadhi mahindi hayo ambayo uzalishaji wake umeongezeka katika kipindi cha mwaka .
“ Serikali imeshatoa fedha hizo ili kuweza kununua tani hizo katika kipindi cha msimu huu”alisema Waziri Wasira huku akifafanua kwamba tayari serikali imeshanunua tani za mahindi 52,000 katika kipindi cha msimu huu hivyo ifikapo mwisho wa mwezi huu ambazo tani za mahindi 105,000 za mahindi zitakuwa zimenunuliwa na Serikali .
Aliongeza pia Serikali itaomba fedha nyingine sh. bilioni 33 kutoka Hazina kwa ajili ya kununua tani za mahindi nyingine za mahindi 95,000 ili kufikisha lengo la awamu ya kwanza ya ununuaji wa mahindi hayo ambayo jumla yake ni tani 200,000.
Hata hivyo aliongeza kwamba baada ya ununuzi huo watafanya tathimini ili kuweza kufikisha lengo la kununua tani nyingine za mahindi 200,000 zilizobakia kama ilivyoagizwa na Rais Kikwete.
Waziri Wasira alisema hifadhi ya Taifa hivi sasa ya ina tani za 52,000 zilizonunuliwa msimu huu na nyingine tani za mahindi za awali 47,000. Hata hivyo alisema uwezo wake wa kuhifadhi ni tani 240,000.
Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa mahindi katika kipindi cha mwaka huu alisema umeongezeka,hivyo hayo ni mafanikio mazuri kutokana na hali ya hewa ilikuwa nzuri.
Alisema katika kipindi cha mwaka huu uzalishaji wa mahindi umeongezeka hadi kufikia tani milioni 4.7 wakati katika kipindi cha mwaka jana ulikuwa tani milioni 3.5.
“ Uzalishaji huu katika kipindi cha mwaka jana ulituwezesha kuwalisha watu milioni mbili wa mikoa yote iiliyokuwa na uhaba wa chakula ya kanda ya Kaskazini bila ya kuagiza chakula toka nje ya nchi au kuomba msaada wa namna hiyo,” alisema Waziri Wasira.
Waziri Wasira alisema tayari wameshafanya maandalizi ya kuagiza mbegu za mahindi tani 20,000, hivyo tani 9000 za mbegu hizo zimeshaagizwa kutoka nchi mbalimbali Tanzania ikiwemo na kampuni zitazipeleka karibu na wakulima. Hhata hivyo alisema mahitaji ya sasa ya mbegu hizo ni tani 30,000.
Kwa upande wa mbolea tani tayari kuna tani 201,000 wakati mahitaji ni tani 385,000, lakini tani nyingine zinaendelea kuagizwa.
Akizungumzia kuhusu ziara aliyoifanya Iran wiki iliyopita, Waziri Wasira alisema itasaidia kutoa ushirikiano katika masuala ya kilimo kati ya nchi hiyo na Tanzania. Hivyo Iran , itawekeza nchini Tanzania kwenye zana na kilimo, umwagiliaji, uongezaji thamani wa mazaokwa kuwekeza viwanda na kufanya utafiti ili kuhamasisha kilimo kwanza katika kukuza viwanda.
Vodacom Tanzania imepunguza gharama zake katika huduma ya kupiga simu, ambapo wateja wa Vodacom wataweza kupiga simu kwenda mitandao mingine nchini kwa punguzo la zaidi ya asilimia 50.Hii ni katika jitihada za kampuni hii kuhakikisha kuwa mawasiliano yanapatikana kwa gharama nafuu, nchi nzima.
Gharama hizi mpya zitamruhusu mteja wa Vodacom kuweza kupiga kwenda mitandao mingine kwa kiasi kidogo cha shilingi tatu tu za kitanzania kwa sekunde, wakati hapo awali gharama ya kupiga simu kwenda mitandao mingine ilikuwa shilingi sita na nusu.
Huduma hii imekuja miezi michache tu baada ya Vodacom kuzindua huduma nyingine ya shilingi moja kwa sekunde , maarufu kama HABARI NDIO HII.
Ikiwa na wateja milioni nane nchini, kampuni ya Vodacom imeendelea kutoa bidhaa na huduma kwa wateja wake,na kuwawezesha kupata mawasiliano kwa gharama nafuu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacon Tanzania, Mwamvita Makamba alisema jana kwamba kuwa gharama hizi mpya zimeleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano ya simu nchini.
“Kama tulivyozindua huduma ya Habari Ndio Hii, tumejikita kuhakikisha kuwa mtandao wetu unatoa bidhaa na huduma bora kwa wateja wetu ili kuwajenga kiuchumi.”
Kampuni ya Vodacom imekuwa nchini kwa miaka kumi sasa na inatabiri kukua zaidi katika sekta hii mwaka huu na miaka mingine ijayo.
“Tutamatumaini makubwa juu ya utendaji wetu hapo mbeleni na tunashauku kubwa kuweza kutoa huduma zetu zenye ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu.”
Huduma zingine za Vodacom kama Vodajamaa na Cheka Time zitabaki kama zilivyo.
“Vodacom inawahakikishia wateja wake kuwa itaendelea kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu hapo mbeleni” Bi Pendaeli alihitimisha kusema.
Wanaume wa Tanzania sasa wanachokitu cha kujivunia kutokana kuanzishwa kwa Jarida la Man ambalo lilianza kuonekana mitaani mwishoni mwa mwaka jana.
Jarida hili limekuwa likigusa mambo mbalimbali yanayohusu wanaume kuanza kwenye afnya, biashara na maisha ya kawaida.
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Euro Consultancy Limited, Dismas Masawe alisema Jarida la Man linachapishwa na wazawa ambapo kwa sasa linapatikana nchini kote na likiwa katika toleo lake la nne.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana uliofanyika kwenye hoteli ya New Africa, Dar es Salaam, Masawe alisema jarida hilo litakuwa linatoka kila baada ya miezi miwili na limeanzishwa ili kuziba pengo lililokuwepo katika sekta ya majarida kutokana na yale yaliyopo kuandika zaidi habari za wanawake.
“Jarida letu linachimbua mambo mbalimbali ambayo msomaji angependa kuyajua kuanzia magari, mambo ya ujenzi, taasisi za fedha, mambo ya uchukuzi, michezo, teknolojia, mitindo, uhusiano na kupitia mambo mbalimbali yanayotuzunguka katika jamii,” alisema.
Massawe, alisema jarida la Man linachapishwa katika kiwanda cha Jamana Dar es Salaam, na kwamba ni sehemu ambayo wanawake wanaweza kutumia kama jiwe muhimu la kuwatambua wanaume na kufahamu nini jinsia nyingine.
Alisema katika matoleo manne ambayo yamekwishatoka mpaka sasa Man limewahoji watu mbalimbali maarufu nchini. Katika toleo la kwanza Man, ilimfanyia mahojiano ndugu Azim Jamal ambaye ni mhamasishaji mkubwa, mchambuzi na mzungumzaji mkubwa. Toleo la pili Nehemiah Kyando Mchechu ambaye alikuwa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika na sasa ni Mtendaji Mkuu wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC).
Katika jarida la tatu Man, ilimhoji Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited, ambaye pia ni Mbunge wa Singida, Mohamed Dewji, na katika toleo la mwisho Man lilimhoji Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Executive Solutions Limited, NduguAggrey Marealle. Marealle aafahamika kwa uwezo wake mkubwa katika kazi za Uhusiano wa Umma na Serikali kwa ujumla.
Massawe alisema Jarida la Man hivi karibuni litafungua milango kwa nchi za jirani za Kenya na Uganda na baadaye Kusini mwa Afrika kutokana na kuwepo kwa soko zuri la katika eneo hilo.
Pia katika siku zijazo, Jarida hili litakuwa likipatikana kwenye mtandao ambapo wasomaji watakuwa na uwezo wa kulipia ili waweze kulisoma.
Kwa mujibu wa Mtendaji huyo, Jarida hilo linawachangiaji wengi ambao wako katika ngazi juu katika serikali na taasisi mbalimbali mpaka raia wa kawaida. Massawe alisema wachangiaji wengine pia ni wanawake.
Aliwataka watanzania kujenga utamaduni wa kusoma ili kuweza kujua mambo mbalimbali yanayotokea duniani na pia kujua vitu mbalimbali.
“Watu wengi hawapendi kujisomea, lakini kusoma ni mojawapo ya njia ya kufanya mtu asiwe na muda kupoteza na pia kujifunza mambo mengi zaidi yanayotokea duniani,” alisema.
Amesema japokuwa Jarida hilo linahusu wanaume, lakini imeonekana wanawake wengi wameonekana kuvutiwa nalo na kulisoma.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na
Dismas Massawe
CEO, Euro Consultancy Limited.
Mobile: 0784407475/0655407475
Email: dismas@eurocom.co.tz
au
Taji Liundi
Chief Editor, Man Magazine,
Mobile: 0787888799