Na. Mary Kweka – MAELEZO.
Dar es Salaam.
Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora imesema itaendelea kulinda, kutetea , na kushughulikia malalamiko mbalimbali ya uvunjwaji wa Haki za binadamu kwa watoto nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Kiongozi Mstaafu Ramadhani Manento wakati akizungumza na viongozi wa mabaraza ya watoto waliofanya ziara ofisi kwake ikiwa ni sehemu ya kongamano lao la mwaka huu linalomalizika leo ( jumamosi) jijini Dar es salaam.
Alisema ili kujenga taifa bora lenye maadili , jamii inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa na kuthaminiwa pamoja na kupatiwa mahitaji mbalimbali yakiwemo Elimu, Malazi bora, haki ya kupendwa, uhuru wa kucheza na kutoa maoni.
Aliongeza kuwa katika kulinda na kutetea haki za watoto, Serikali kupitia tume ya haki za binadamu na Utawala Bora imeanzisha Dawati la watoto ambalo linawajibika na kupokea malalamiko mbalimbali ya uvunjwaji wa haki za biadamu kwa watoto.
“Dawati la watoto linawajibika kulinda na kutetea haki za watoto wanaoishi katika mazingira magumu, walioachishwa shule,matatizo ya miradhi, utekelezaji wa sheria ya ubakaji wa watoto kwa watuhumiwa na mazingira ya watoto walio magerezani “Alifafanua Jaji Manento.
Aliendelea kufafanua kuwa Dawati hilo linatoa elimu kwa watu hasa wazazi kutambua umuhimu wa haki za watoto na kuwa makini pale wanapotoa adhabu kwa watoto huku akitoa angalizo kwa wazazi kuwa makini na adhabu hizo kuwa ziwe na vikomo na si zakuwajeruhi watoto na kuwasababishia ulemavu na kuwapotezea maisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti na Nyaraka wa tume hiyo Bi Epifania Mfundo alisema mwaka huu dawati la watoto limepokea jumla ya malalamiko 114 mpaka sasa, na wamefanikiwa kushughulikia malalamiko 28 kati ya 114 yaliyowasilishwa kwenye tume ya haki za binadamu na utawala bora.
No comments:
Post a Comment