Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania Hemed Mkali(katikati) akitangaza leo jijini Dar es salaam ufunguzi wa ununuzi wa korosho hapa nchini kwa msimu wa 2010/2011. Wengine ni Mkurugenzi wa Huduma za Masoko wa Bodi hiyo Mohamed Hassan Hanga (kushoto) na Meneja Tawi wa Bodi Tawi la Dar es salaam Martin Malifedha.
NA ZAHRA MAJID- MAELEZO.
MSIMU wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2010/2011 nchini unatarajiwa kuanza Jumatano ya wiki.
Ununuzi huo unatarajia kutumia Mfumo wa Stakabadhi ghalani ambapo Vyama vya Ushirika vitapeleka korosho kwenye maghala ya Serikali ambapo ndipo mnada utafanyikia.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar-es-salaam na Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Hemedi Mkali wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari ( MAELEZO).
Alisema kuwa korosho zitauzwa kwa mnada utakaofanyika katika Bodi ya Korosho na katika Ofisi za Bodi katika mikoani Tanga, Mtwara, Pwani, Dar-es salaam, Morogoro, Ruvuma na Wilaya za Kyela na Ludewa Tunduru.
Mkali alisema kuwa korosho zitakazouzwa ni zile tu zitakazokuwa kwenye magulio yaliyosajiliwa na Serikali na kuongeza uuzaji wa korosho kinyume cha utaratibu huo , wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria namba 12 ya mwaka 2009.
“ Wanunuzi wa korosho wanaombwa wafuate taratibu hizi za ununuzi kwani watakaojaribu kukiuka taratibu hizi za ununuzi basi wajue Sheria hii inayohusu sekta ya korosho itachukua mkondo wake” Mkali alisema.
Mkali alizitaja kuwa timu zitakazoendesha mnada huo kuwa na wawakilishi toka Bodi ya Korosho,Vyama vya Ushirika Benki ya CRDB na NMB, Bodi ya Leseni za maghala Tanzania, Maafisa Ushirika watakaoteuliwa kama waalikwa na wengine wanaohitaji kushuhudia watafuata utaratibu maalum wa minada hiyo.
Halikadhalika, alisema kuwa,katika mfumo wa stakabadhi za mazao maghalani, kwa niaba ya wakulima korosho zitakusanywa na chama cha ushirika cha msingi katika magulio yaliyosajiliwa kwa kuwalipa wakulima asilimia 70 ya bei dira kwa korosho daraja la kwanza.
Mkali alisema kuwa watalipwa malipo ya pili asilimia 30 baada ya korosho kuuzwa mnadani.
“Aidha watalipwa malipo ya tatu (ya majaliwa) kutokana na bei itakayopatikana kwenye mauzo mnadani” Aliongeza Mkali.
Mkali alitaja viwango vya bei za korosho kuwa ni Tshs. 800 kwa kilo moja kwa daraja la kwanza(STD) na Tshs. 640 kwa kilo moja kwa daraja la pili(UG).