Aug 27, 2010

NHIF YAWATAKA VIONGOZI TALGWU KUTHIBITISHA MADAI

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya akitoa ufafanuzi kuhusu madai yaliyowasilishwa kwenye vyombo vya habari na viongozi wa Talgwu kuwa wanadai serikali na Mfuko wakati alipokutana na waandishi wa vyombo mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa mfuko huo kurasini bendera tatu kushoto kwake ni wakurugenzi wa mfuko.

Na.Paul Marenga NHIF
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekitaka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kutokwepa kueleza ukweli kuhusiana na madai ya makato yaliyokatwa kimakosa kwa wanachama wao wakati wa uanzishaji wa Mfuko huo mwaka 2001.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Mfuko huo Bendera Tatu, Dar es salaam leo.

“Sisi katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hatutaki malumbano, bali tunapenda kupitia kwenu umma wa Watanzania na wanachama wetu waelewe ukweli kuhusu suala hili ambalo kwanza siyo suala geni,” alisema Humba.

Mfuko huo uliamua kutoa ufafanuzi baada ya baadhi ya vyombo vya habari juzi na jana kutangaza na kuandika kwamba Talgwu itaifikisha mahakamani NHIF kwa kushindwa kulipa wafanyakazi 58,000 wa Tamisemi zaidi ya sh bilioni 3.6 ambazo zilikatwa kinyume cha sheria.

Alisema pamoja na ukweli kwamba madai haya yamekuwa yakitolewa au kuibuka kunapokuwa na uchaguzi ndani ya TALGWU au uchaguzi mkuu wa Serikali, viongozi wa TALGWU wamekuwa hawawaambii wanachama wao maagizo ya serikali kuhusiana na madai yao hayo.

Yapo maagizo ya Serikali katika suala hili, alisema Humba na kuongeza kuwa TALGWU ilipaswa kueleza wazi imefanya nini ili kulimaliza kabisa suala hili ambalo Mfuko tayari ulishatekeleza kwa upande wake, kulingana na maagizo na miongozi ya Serikali.

Kwa mujibu wa Humba, Serikali na NHIF baada ya kubaini kuwa kulikuwa na Watumishi 12,894 waliokatwa kimakosa iliwarejeshea kiasi cha Shilingi 269,563,469.54 watumishi hao.

Alisema kazi ya kuwakabidhi fedha hizo ilifanywa kwa pamoja kati ya Mfuko na Chama cha TALGWU makao makuu na matawi yake mikoani.

Akifafanua zaidi alisema pamoja na hatua hiyo ya kuwalipa watumishi hao, TALGWU ilikuja na madai mapya wakisema bado kuna watumishi 53, 000 ambao hawajalipwa na wanadai kiasi cha Shilingi bilioni 1.8 na sasa wanadai shilingi Bilioni 3.6 kwa watumishi 58,000.

“Kwa taasisi yoyote inayofuata misingi ya fedha taratibu lazima ziwepo na hawa kama wanaona kwamba malipo ya mwanzo hayatoshi basi wafuate maagizo yanayostahili.

“Hakuna wakati wowote ambapo Mfuko huu umekaidi kutekeleza maelezo yoyote halali, kama TALGWU wanavyodai katika taarifa yao iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari jana,” alisema.

Mwongozo wa pili wa makato ya wafanyakazi kwenda NHIF kutoka Utumishi uliotolewa Mei 2002, ulifafanua kuwa wanaokatwa ni wale wanaolipwa na Serikali kuu ingawa walikuwa katika Serikali za Mitaa na kubainisha kuwa watumishi ambao hawahusiki na makato ni wale walioajiriwa na Serikali za mitaa na kulipwa kwa kutumia vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa.

Hata hivyo Serikali, Mwezi Novemba, 2002 illifanyia mapitio Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuwajumuisha Watumishi wote walioko kwenye Serikali za Mitaa.

Humba alisema chimbuko la madai ya TALGWU ni kuwa wao hawaikubali tafsiri iliyotolewa na Serikali kuhusu ni nani waliotakiwa kuchangia na vilevile haikubali miongozo ya makato iliyotolewa na Serikali, jambo ambalo liko nje ya uwezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

“Tunauomba uongozi wa TALGWU kama kuna madai yoyote halali basi wafuate maelekezo waliyopewa ya kuwasilisha orodha ya majina ya watumishi wanaodai kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na yakishahakikiwa na kuletwa kwetu, sisi tutawalipa mara moja,” Alisema Humba.

Alisema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakati wote unafanya kazi zake kwa kuzingatia Sheria ya kuundwa kwake na kusimamia majukumu yake kwa mujibu wa Sheria. “Fedha hizi ambazo tunazisimamia ni fedha za umma (Public Funds) ambazo zinasimamiwa na kukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Ndiyo maana hata malipo ya awali tuliyalipa kwa kuzingatia taratibu za fedha na idhini kutoka Serikalini.” Alisema.

No comments:

THE DON HIMSELF

Karibuni sana kwenye blog hii ya kijamii iliyosheheni makila kitu kuanzia siasa uchumi afya na burudani kwa ujumla wake.uingiapo kwenye blog hii ni mengi ambayo utapata nafasi ya kukutana nayo,kumbuka mawazo yako ndo hasa yanayojenga na kunifanya niwe na ufanisi zaidi.kariiiiiiibuuuuuuuuuuuu saaaaaaaaaaaaaaanaaaaaaaaaa.(THE DJ HIMSELF-JIWE)

Followers

BLOG ZA MARAFIKI

Search This Blog

ZILIZOPITA

DUNIA MUZIMA