Oct 9, 2010

Rais Kikwete aongea na wana CCM Wilaya ya Ilala!

Msanii kutoka katika kikundi cha Survival Sisters Lucy Samson akimkabidhi Rais Jakaya Kikwete kazi yao ya sanaa muda mfupi kabla ya Dr.Kikwete kuwahutubia wanachama wa CCM kutoka wilaya ya ilala katika ukumbi wa PTA viwanja vya maonyesho Sababa jijini Dar es Salaam leo asubuhi.Wengine ni Irene Malekela(kushoto) na Latifa Abdalah.
Wanachama wa CCM Wilaya ya Ilala wakimshangili mgombea uraius kwa tiketi ya CCM

Dr.Jakaya Mrisho Kikwete alipowahutubia katika ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar es Salaam leo mchana(Picha na Freddy Maro)

MAMA SALMA KIKWETE AONYA WANAOFANYA KAMPENI KWA KUTUMIA UKABILA NA UDINI!!

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amesema kufanya kampeni kwa kutumia udini na ukabila ni kuhatarisha amani.

Alisema hayo juzi na jana alipozungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani hapa, alipokuwa akiwaombea kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Mama Salma alisema kuwagawa Watanzania kwa misingi ya udini na ukabila ni kutaka kutowesha amani ambayo imedumu nchini kwa miaka mingi.

“Udini na ukabila utatutenganisha, tutahasimiana kwa sababu huyu ni mkristo na yule ni muislamu, haya ni yale yale ya huyu ni Mtutsi na yule ni Mhutu, jamani kina mama huko ndiko tunataka kwenda ?” Alihoji na kujibiwa “hapana”.

Mama Salma alisema, wanachama wa vyama vya siasa wana dini zao, lakini usajili wa vyama hivyo haufanyiki kwa kuangalia dini na kabila, hivyo kufanya kampeni kwa vigezo hivyo ni ukiukaji wa sheria.

Wakati akizungumzia hilo, kina mama hao walikuwa wakimwitikia kwa kusema “sema mama usiogope” kuashiria kuna baadhi ya watu wanafanya kampeni za kibaguzi kwa kutumia udini na ukabila.

Mwenyekiti huyo wa WAMA ambaye ni mke wa mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alitahadharisha kwamba, amani kuvunjika ni rahisi, kuirejesha ni kazi kubwa na mifano ipo katika baadhi ya nchi za Afrika ambazo ziliichezea na haijarejea.

Aliwaambia wananchi wa Kigoma kwamba wao ni mashahidi wa namna nchi jirani zilivyoathirika kutokana na machafuko chanzo kikiwa ni siasa za kibaguzi zilizojiegemeza kwenye udini na ukabila.

Mama Salma aliwaombea kura wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM; Injinia Christopher Chiza (Buyungu), Jamal Tamimu (Muhambwe), Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Vijijini), Raphael Neka (Kasulu Mjini), Robson Lembo (Kigoma Kaskazini), Peter Serukamba (Kigoma Mjini) na Gulamuhussein Kifu (Kigoma Kusini).

Diamond Kutua UK November 2010!

Urban Pulse Creative ikishirikiana na Aset Inapenda kuwataarifu wadau wote wa Music wa bongo Flava na Hip Hop kuwa imeandaa tamasha maalum linaloitwa URBAN TOUR ambapo msanii Diamond kutoka bongo anayetamba na kibao chake cha Mbagala atakuwepo hapa ukerewere kuanzia mwezi wa November mwaka huu. Wasanii wengine ni Pamoja na First lady wa Urban Pulse Mish Ze Fyah Sis UK Artist anayetamba na single yake Freedom na I don't give a damn.

Jakaya Kikwete atimiza miaka 60 ya kuzaliwa kwake!!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikata keki wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 60 tangu kuzaliwa kwake pembeni yake ni Mama salma Kikwete na mjukuu wao Karima wakishuhudia.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimlisha kipande cha keki mkewe Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe ya kuadhimisha kuzaliwa kwake miaka 60 iliyopita.Sherehe hizi zilifanyika katika viwanja vya ikulu jijini Dar es Salaam jana usiku.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimlisha kipande cha keki Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa sherehe ya kumpongeza Rais Kikwete kwa kutimiza miaka 60 ya kuzaliwa kwake jana jioni.Sherehe hizo zilifanyika katika viwanja vya ikulu jijini Dar es Salaam(picha na Freddy Maro)

JAJI MFAWIDHI ERNEST MWAIPOPO AAGWA RASMI LEO JIJINI DAR ES SALAAM!!

Jopo la majaji wa mahakama kuu wakiongozwa na jaji Kiongozi Fakihi Jundu (katikati) wakimuaga rasmi kitaaluma na kwa heshima jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Mahakama ya Kazi ya Mahakama Kuu, Ernest Mwaipopo (wa tano kutoka kulia mstari wa mbele) ambaye amemaliza muda wake wa kulitumikia taifa leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya majaji wa mahakama kuu wakifuatilia kwa makini baadhi ya kumbukumbu ya maamuzi ya kesi yaliyowahi kutolewa na jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Mahakama ya Kazi ya Mahakama Kuu, Ernest Mwaipopo kipindi cha utumishi wake wakati wa hafla ya kumuaga rasmi kitaaluma leo jijini Dar es salaam.

Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Mahakama ya Kazi ya Mahakama Kuu, Ernest Mwaipopo akizungumza na majaji,mawakili , wageni waalikwa na wadau mbalimbali wa sheria wakati wa hafla ya kumuaga rasmi kitaaluma iliyofanyika mahakama kuu leo jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine ametoa wito wa kufanyika kwa utaratibu wa shughuli za mahakama zikiwemo uandikaji wa hukumu na mienendo ya kesi kutumia lugha ya kiswahili ambayo inatumiwa na kueleweka miongoni mwa wananchi.

Majaji wa mahakama kuu na wasajili wa mahakama (waliovaa suti nyeusi) wakifuatilia kwa makini baadhi ya kumbukumbu ya maamuzi ya kesi yaliyowahi kutolewa na jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Mahakama ya Kazi ya Mahakama Kuu, Ernest Mwaipopo yaliyokuwa yakisomwa na jaji kiongozi Fakihi Jundu wakati wa hafla ya kumuaga rasmi kitaaluma leo jijini Dar es salaam.
Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Mahakama ya Kazi ya Mahakama Kuu, aliyemaliza muda wake Ernest Mwaipopo akiwa katika picha ya pamoja na majaji wa mahakama kuu mara baada hafla ya kumuaga leo jijini Dar es salaam.

MSIMAMO WA WAHARIRI WA HABARI ZA MICHEZO KUHUSU UINGIAJI MECHI YA STARS V MOROCCO

LEO Ijumaa Oktoba 8, wahariri 37 wa habari za michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari walikutana mgahawa wa Hadee’s jijini Dar es Salaam kuzungumzia masuala ya uingiaji wa waandishi wa habari kwenye mchezo wa kesho kati ya Taifa Stars na Morocco.

Kama tunavyofahamu ni kuwa TFF imetangaza kwamba itatoa tiketi maalum mchezo wa Taifa Stars na Morocco, badala ya kadi ambazo zimekuwa zikitumika katika michezo mbalimbali ya ligi.

Kutokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wanahabari za michezo kupinga uamuzi huo wa TFF, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kiliitisha mkutano na wahariri wa habari za michezo.

Mambo mbalimbali yalizungumzwa, huku malalamiko yakiwa mengi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linawanyanyasa waandishi wa habari na kuwatumia pale tu linapokuwa na maslahi yake.

Msimamo wa kikao ni kuwa kadi za TFF zinazotumika kwenye michezo mbalimbali si nyingi kama wengi wanavyodhania, na kwamba ingawa TFF inasema ilitoa kadi 170 mwaka 2008, idadi halisi ya wanaofanya kazi hiyo hawafikii hata 100.

Kwa misingi hiyo wajumbe wa kikao walikubaliana kwamba TFF itamke kuwa waandishi wa habari za michezo waruhusiwe kutumia kadi hizo kwa sababu wapo wanaoenda kwenye mechi kwa ajili ya kuripoti mpira, wengine kuandika makala, wengine kupiga picha na wengine matukio ya kawaida yasiyohusiana na mchezo wa uwanjani.

Mjumbe mwalikwa wa kikao hicho, Florian Kaijage ambaye ni Ofisa Habari wa TFF, alipopewa nafasi ya kuzungumza aliwaeleza wahariri kuwa tayari utaratibu uliokuwa umepangwa ni kuwa hakuna atakayepita mlangoni bila kuwa na tiketi.

Hivyo aliwaeleza wajumbe hata kama watakubaliana zitumike kadi, italeta vurugu kwenye majukwaa kwa sababu tiketi zina namba za viti.

Kaijage alipewa fursa ya kusikiliza hoja mbalimbali na mwishoni aliombwa na kikao aendelee na shughuli zake, lakini msimamo ukiwa wahariri wanataka zitumike kadi na si vinginevyo.

Hata hivyo baada ya majadiliano ya muda mrefu, kujali utaifa pamoja na busara za kiuhariri tulikubaliana yafuatayo:

    1. Kwa kuwa TASWA na Wahariri wanaamini TFF imekuwa ikifaidika zaidi na vyombo vya habari kwa kuandikiwa habari zao nyingi ambazo nyingine ni promosheni, kuna haja ikawathamini katika hili.

      TASWA na Wahariri wanaamini kwa kuwa idadi ya waandishi wanakaoingia uwanjani ni chache tofauti na wengi wanavyofikiri, na pia wengi wa waliopewa kadi mwaka 2008 hivi sasa karibu 50 hawapo kwenye vyombo vya habari na TFF haina haja ya kuogopa hilo.

    1. Lakini kwa sababu TFF inasema ukaaji uwanjani utahusu namba za viti, basi TFF itenge tiketi 120 kwa ajili ya wanahabari.

      Tiketi hizo zitasimamiwa na Ofisa Habari wa TFF kwa kushirikiana wa Wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, ambao ni Mhazini Sultani Sikilo na Mjumbe Grace Hoka.

      Hawa watazigawa tiketi hizo kwa wote watakaokuwa na kadi za TFF za kuingia uwanjani zilizotolewa mwaka 2008.

      Hivyo kitakachofanyika ni kwa mhusika kuonesha kadi yake ya TFF atapewa tiketi ya Taifa Stars na Morocco ili aingie uwanjani.

      Hili litasaidia pia kudhibiti wale ambao hawapo kwenye vyombo vya habari, lakini wanamiliki vitambulisho, pia kuwa na uhakika wa namba halisi ya wenye vitambulisho badala ya hiyo ya TFF ambayo inaonekana si sahihi.

      Hivyo kama hilo litakubaliwa waandishi wa habari za michezo wataombwa kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa 6 mchama wafike ofisi za TFF Uwanja wa Karume, Dar es Salaam ili wapewe tiketi lakini kwanza waoneshe hizo kadi za TFF.

(4)Viongozi wa TASWA wawasiliane na TFF wawaeleze msimamo huu na kama itatokea wenye kadi wakazidi idadi ya tiketi, hilo litafanyiwa kazi na busara itatumika kati ya TASWA na TFF ili kila anayestahili aweze kufika uwanjani.

Hata hivyo angalizo la wahariri ni kuwa wale ambao wanaelewa hawapo kwenye vyombo vya habari kwa sasa, hata kama wanazo kadi za kuingia uwanjani, wasiende maana hawatapewa tiketi na badala yake kadi zao zitazuiwa.

MSIMAMO:

Kama TFF ikishindwa kutekeleza hayo mapendekezo basi yafuatayo yatafanyika:

(1)Tiketi 70 ilizopanga TFF kutoa kwa ajili ya wanahabari hazitachukuliwa na mwandishi yeyote, badala yake TFF wazitumie wenyewe kadri watakavyoona inafaa wenyewe.

(2)Vyombo vya habari vigharamie watu wake kwenda kuripoti mechi hiyo, bila kujihusisha kwa namna yoyote na TFF.

(3)Waandishi wa habari hawatajihusisha na kuandika habari za TFF zinahusu promosheni ya aina yoyote, isipokuwa habari ambazo ni za maslahi kwa Taifa ikiwemo mechi za timu za Taifa.

Lakini masuala mengine ya TFF, ikiwemo kutangaza viingilio, adhabu za waamuzi ama hata kupata udhamini wa kitu fulani, wahariri wamekubaliana kwamba hilo halitafanywa.

Pia hata upigaji picha viwanjani katika maeneo ambayo ni kuitangaza TFF hayo hayatapewa nafasi.

Masuala mengine muhimu juu ya nini kifanyike wahariri wamekubaliana tena wakutane Jumatano wiki ijayo kujadili tena mambo mengine ya kufanya, ikiwa ni pamoja na utaratibu mzuri wa waandishi kuingia uwanjani na kufanya kazi zao bila bugudha.

Karibu vyombo vyote vya habari vilishiriki kwenye mkutano huo, ambao wengi waliupongeza uongozi wa TASWA kwamba ni mwanzo mzuri.

Amir Mhando

Katibu Mkuu TASWA

08/10/2010

TFF REKEBISHENI HILI KWA MANUFAA YA JAMII KUPATA HABARI!!

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini TASWA Juma Pinto kulia akimsikiliza kwa makini Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini Frolian Kaijage wakati wa kikao maalum kilichkokuwa kikijadili utaratibu mbovu ambao umekuwa ukitumiwa na TFF katika kuruhusu waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kufanya shughuli zao katika matukio mbalimbali ya michezo ya kimataifa inayofanyika hapa nchini kati ya timu ya taifa Taifa Stars na timu mbalimbali za nje. TFF imekuwa ikilazimisha kutoa tiketi kwa waandishi wa habari pamoja na waandishi hao kuwa na vitambulisho vilivyotolewa na shirikisho hilo kwa waandishi ambavyo vinatambulika na Shirikisho hilo. Utaratibu huo wa TFF umekuwa ukiwakwamisha wanahabari kufanya kazi yao huku wakinyanyaswa na vyombo vya dola kama vile kupigwa na kusukumwa hovyo huku wengine wakizuiwa milangoni bia kuingia uwanjani kwa ajili ya kuripoti michezo hiyo. Kumekuwa na adha kubwa hasa mara timu ngeni zinapowasili nchini kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu J.K.Nyerere hasa kwa wapiga picha, kwani wamekuwa wakizuiwa kufanya kazi yao, utaratibu wa kufanya kazi kuwa mbovu kiasi kwamba kazi inakuwa ngumu sana kuifanya Nasema hivi kwakuwa mimi nilikuwa mmoja wa wapigapicha waliopata shida sana wakati timu ya Ivory Coast ilipokuja hapa nyumbani kwa mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya timu yetu Taifa Stars, ilikuwa ni kazi ngumu na kulitokea purukushani kiasi kwamba Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Mh.Joel Bendera aliingilia kati na kuzungumza na waandishi wa habari kwenye uwanja wa ndege wa J.K.Nyerere akiwaomba waendelee na kazi yao baada ya kuletewa purukushani za hapa na pale na wanausalama. Juzi ilipowasili timu ya Taifa ya Moroco pia jambo hilo limejitokeza ambapo tulizuiwa kwa muda mrefu kuingia kwenye uwanja huo, kitu kilichozua malalamiko kwa wanahabari, lakini jibu lililotoka kwa wanausalama walisema wao hawana tatizo isipokuwa wamepokea maelekezo kutoka juu, tuliendelea kusota mpaka wachezaji walipoanza kuingia kwenye basi ndipo tukaruhusiwa kuingia kitu kilichofanya tukose baadhi ya picha muhimu tulizokuwa tukizihitaji. Kitu hiki kinaifanya niilaumu TFF kwa utaratibu mbovu wa kuwapanga wanahabari ili kuweza kuripoti vyema matukio hayo kwa faida yao wenyewe na jamii ili iweze kujua kinachoendelea. hili ni jambo la kukaa pamoja kati ya TFF, POLISI na TASWA ili kupanga utaratibu mzuri ambao utawafanya waandishi nao kufanya kazi vizuri bila matatizo na kujiona kama na wao ni sehemu muhimu na kiungo muhimu kwa jamii katika kupata habari.
Msemajiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini TFF Frolian Kaijage akijadiliana jambo kwa msisitizo na Viongozi wa Chama Cha waandishi wa habari za Michezo nchini TASWA wakati wa majadiliano kati ya shirikisho hilo na Taswa leo mchana kuhusua utaratibu wa waandishi wa habari kuingia uwanjani kwa ajili ya kuripoti mchezo kati ya Taifa Stars na Moroco, kulia ni Mwenyekiti wa TASWA Juma Pinto na katikati nia Katibu Mkuu wa Chama hicho Amir Mhando.
Wahaariri mbalimbali wakiwa katika kikao hicho leo.
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika mkutano wao wa kujadili mambo mbalimbali ambayo waandishi wa habari wanafanyiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini TFF katika michezo ya kimataifa dhidi ya timu ya Taifa na mambo mengine mbalimbali.

MATAIFA YA AFRIKA YAHIMIZWA KUJIUNGA NA SEAMIC KUENDELEZA MADINI!!

MATAIFA ya Bara la Afrika yametakiwa kujiunga na Kituo cha Utafiti na Uendelezaji wa Sekta ya Madini Kusini na Mashariki mwa Afrika(SEAMIC) ili kuhimili mahitaji yaliyopo katika sekta ya madini katika nchi zao.

Hayo yamesema leo na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakati alipokuwa akipokea hati ya utambulisho ya uanachama wa Sudani katika SEAMIC Jijini Dar-Es-Salaam.

Waziri Ngeleja alisema mataifa ya Afrika yamekuwa yakitumia gharama kubwa ya rasilimali fedha katika usafirishaji wa sampuli za madini kwa ajili ya utafiti wa kimaabara katika nchi za nje pasipo na kuitumia fursa ya SEAMIC, ambayo imeweka wazi dhamira yake katika kuongeza ufanisi wa shughuli za madini.

Kwa mujibu wa Waziri Ngeleja anasema tangu SEAMIC ianze shughuli zake hapa nchini mwaka 1997, Tanzania imeweza kufanya utafiti wa sampuli 35000 za madini, na hivyo kulifanya taifa kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za usafirishaji wa sampuli hizo nje ya nchi..

“Kama tutakuwa na wanachama wengi wa SEAMIC itasaidia mataifa yetu ya Afrika kumudu changamoto mbalimbali katika sekta ya madini ikiwemo rasilimali fedha na kuongeza ufanisi, hivyo ni wito kwa mataifa yote kushirikiana nao kwa kuzingatia kuwa mwanachama anaweza kujiunga kwa wakati wowote”.

Aidha Waziri Ngeleja alisema SEAMIC pamoja na majukumu mengine imedhamiria kuongeza maarifa katika usimamizi wa madini, kubadilisha takwimu za madini, kuongeza ubora wa madini na kufanya utafiti wa kimaabara kwa sampuli mbalimbali za madini.

Waziri Ngeleja anaongeza kuwa SEAMIC pia imeeleza nguvu zake katika kusaidia wazalishaji wadogo wa madini katika maeneo mbalimbali, ili kuhakikisha kuwa wachimbaji hao wananufaika na shughuli hizo zinawaongezea tija na ufanisi mkubwa zaidi.

Naye Balozi wa Sudan hapa nchini, Abdel-Bagi H. Kabeir anasema, Serikali yake itatumia vyema fursa ya uanachama wa SEAMIC kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wote wa Sudan na Bara la Afrika kwa ujumla wake, kwani nchi hiyo imebahatika kuwa na rasilimali nyingi katika sekta ya madini na nishati.

Tumejiandaa kikamilifu katika kuhakikisha kuwa fursa ya uanachama huu inatumika kikamilifu katika nchi yetu na hilo litaweza kuonekana katika kipindi kifupi kijacho” anasema Balozi Kabeir

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa SEAMIC, Bw. Katema Tadesse anasema tangu taasisi hiyo iingie nchini jumla ya wachimbaji wadogo 500 wameweza kupewa mafunzo katika namna ya kuendesha shughuli za madini, ikiwemo kutafuta masoko na kuongeza thamani ya madini katika maeneo yao ya uzalishaji.

Tadesse anasema uanachama wa SEAMIC upo wazi kwa kila nchi za Afrika, hivyo kutoa fursa hiyo ina yenye manufaa kwa kuwa shughuli zake zitasaidia mataifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo mafunzo, uzalishaji, uchimbaji wenye kuzingatia utunzaji wa mazingira, utafiti wa kimaabara wa sampuli za madini.

DK. GHALIB BILAL AKIWA KITETO JANA!!

Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, DK. Mohamed Gharib Bilal, akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Kijungu Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini hapo jana jioni Okt 7.
Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Dk. Mohamed Gharib Bilal, akimnadi mgombea Ubunge wa Jimbo la Kiteto, Benedict ole Nangolo, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara jana Okt 7.
Wananchi wa Kijiji cha Kijungu (Wamasai) wakimsikiliza Mgombea Mwenza wa urais wa CCM, DK. Mohamed Gharib Bilal wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini hapo jana Okt 7, Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara.
Wananchi wa Kijiji cha Kijungu Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara, wakimsikiliza mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipokuwa akiwahutubia wananchi hao katika mkutano wa kampeni jana jioni

Oct 7, 2010

Katibu Mkuu Habari akemea vyombo vya habari vinavyoandika habari za uchochezi!!

Serikali imeonya vyombo vya habari kuacha mara moja kuandika habari za uchochezi unaolenga kuwachonganisha wananchi na Serikali yao iliyopo madarakani.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Bw.Sethi Kamuhanda wakati mkutano wake na wafanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Tanzania(TSN) kwenye ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kujifunza shughuli mbalimbali zinazoendeshwa na kampuni hiyo.

Alisema kuwa ni vema vyombo vya habari vikafanya kazi hapa nchini kutoa habari zinazozingatia weledi wa taaluma ya uandishi wa habari na sio kupandikiza uchochezi miongoni mwa Watanzania na hivyo kuzorotesha amani.

Kamuhanda alisema kuwa Serikali haitavumilia hali ya uchochezi inayofanywa na baadhi ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa wageni na vile vya ndani vinavyopandikiza chuki na kuichafua Tanzania.

"Tunaomba vyombo vya habari vyote ambavyo vimefanya uchochezi kuwa sehemu ya professional kuacha mara moja kwani wakitulazimisha tuvifungia au kufuta katika usajili ...tunawaomba kuandika habari ambazo hazina uchochezi na zinazozingatia taratibu na Sheria zilzopo" alisisitiza Katibu Mkuu huyo.

Alisema kuwa pamoja na uhuru uliopo kwa vyombo vya habari nchini ni vema wakautumia vizuri badala ya kugeuza vyombo vya habari kuwa uwanja wa uchochezi unaotishia amani.

Kamuhanda alitoa mfano kuwa kuwa baadhi ya Nchi zijikuta katika machafuko na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya vyombo vya habari vilivyofanya uchochezi kuwa kama ajenda yao kubwa na kuongeza kuwa Serikali halifumbia macho chombo cha habari chenye mlengo huo.

Hata hivyo alisema Serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na kusajili vingine vingi ili cha msingi kwa waandishi wa habari ni kuzingatia weledi wa uandishi wa habari ili uhuru huo ulete maana halisi.

Kwa upande wa wananchi walitoa maoni yao kuhusu agizo hilo la Katibu Mkuu walisema kuwa tamko hilo ni vema likaanza kutekelezwa kwani wamechochosa na baadhi ya vyombo vya habari kugeuzwa majukwaa ya kupandikiza chuki katik ya kundi moja na lingine.

WAZIRI MKUU AZINDUA MRADI WA MATREKTA LUGALO

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua trekta aina Farmtruck kutoka India wakati alipozindua Mradi wa Matrekta ya Kilimo Kwanza unaosimamiwa na JKT SUMA kwenye eneo la kambi ya jeshi ya Lugalo jijini Dar es salaam Oktoba 7, 2010. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akiendesha trekta aina ya FARMTRUCK kutoka India wakati alipozindua Mradi wa Matrekta ya Kilimo Kwanza unaosimamiwa na SUMA JKT, kwenye eneo la Kambi ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es salaam Oktoba 7, 2010. Kulia ni Balozi wa India nchini,V. Bhagirathi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

TAMKO LA KAMATI YA UTENDAJI YA TASWA KUHUSU UINGIAJI UWANJANI MECHI YA MOROCCO V TAIFA STARS

CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimesikitishwa na hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza itatoa tiketi kwenye mechi ya Taifa Stars na Morocco badala ya kadi ambazo zimekuwa zikitumika karibu kila mechi kubwa.

Hatua hii ya TFF tunaiona kama ni ubaguzi na pia kutaka kuwagawa waandishi wa habari za michezo maana walio wengi watakosa kwenda kushuhudia mchezo huu, licha ya juhudi kubwa walizofanya katika kuutangaza kwa umma.

TASWA hailazimishi waandishi wa habari waingie wote, lakini inasikitishwa na namna wanavyonyanyaswa hasa linapokuja suala la mechi kubwa zinazofanyika Uwanja Taifa Dar es Salaam.

Sote tunakumbuka tukio la Juni mwaka huu wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Brazil ambayo waandishi walio wengi walishindwa kuingia uwanjani kutokana na utaratibu ambao haukuwa mzuri, na ulioleta malalamiko kwa wanachama wetu.

Kwa kutambua hili uongozi mpya wa TASWA ulipoingia madarakani Agosti 15 mwaka huu, siku mbili baadaye yaani Agosti 17 Siku ya Jumanne saa tano asubuhi, ujumbe wa viongozi watatu wa juu wa TASWA ulienda ofisi za TFF Uwanja wa Karume Dar es Salaam kujitambulisha na pia kuzungumza masuala mbalimbali yahusiyo waandishi wa michezo na namna ya kuingia uwanjani.

Upande wa TASWA waliohudhuria walikuwa ni Mwenyekiti, Juma Pinto, Makamu Mwenyekiti, Maulid Kitenge na Katibu Mkuu, Amir Mhando, wakati upande wa TFF uliwakilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Athumani Nyamlani, Kaimu Katibu Mkuu, Sunday Kayuni, Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage na Wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji, Eliud Mvella na Muhsin Said.

Ikumbukwe kikao hiki kilifanyika siku moja kabla ya mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga, hivyo tulijadiliana kwa kirefu namna ya waandishi kuingia uwanjani hasa tukirejea tukio la mechi ya Stars na Brazil.

Kwenye mjadala huo tulikubaliana kwamba wakati utaratibu mwingine ukiandaliwa ambao utaridhiwa na pande zote mbili yaani TASWA kama wawakilishi wa waandishi wa habari za michezo na TFF kama wasimamizi wa mpira nchini, zitumike kadi ambazo TFF ilizitoa miaka miwili iliyopita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kuepusha usumbufu kwani zinatumika kwenye ligi.

Tulifikia uamuzi huo wa kutumia kadi kwa kuwa TFF ndiyo iliyozitoa na si nyingi kama wengi wanavyofikiria, mjadala ulikuwa mbona mechi nyingine huwa zinatumika? Hivyo kikao kikaazimia kwamba zitumike kadi hizo na hilo likafanyika na limekuwa likifanyika.

Mambo mengine ikiwemo suala la ukaaji wa waandishi wa habari uwanjani lilizungumzwa lakini ikaonekana kwa Uwanja wa Uhuru TFF wakasema hawana mamlaka nalo, lakini tukapeana muda wa kulitafutia ufumbuzi.

Hili la namna ya ukaaji uwanjani napenda tuseme wakati TASWA mpya ilipoenda kujitambulisha kwa Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo na aliahidi kwamba kwa kushirikiana na TFF watalifanyia kazi.Hivyo hatuna wasiwasi nalo.

Lakini TASWA imesikitishwa sana na kauli iliyotolewa na uongozi wa TFF kwamba watatoa tiketi badala ya zile kadi zao ambazo ndizo waandishi wanatumia iwe mechi ya Stars au timu nyingine yoyote maana kwetu tuliona ndizo 'ACCREDITATION' za TFF viwanjani.

Tunashangaa kwamba TFF kwa makusudi imeamua kuyaweka kapuni yale tuliyozungumza kwenye kikao cha Agosti 17 na kwa kweli hili ni jambo ambalo halipaswi kufanywa na watu wanaofanya kazi kwa pamoja, sisi tukiwa wadau wakubwa wa TFF.

Tunachokiona hapa TFF ina huruma ya mamba, ambaye anakutafuna huku anatoa machozi ukidhani kwamba anakuonea huruma kumbe ndiyo staili yake ya kukumaliza.

Kwa msingi huo Taswa haipo tayari na haikubaliani na utaratibu wa utoaji kadi uliotangazwa na TFF badala yake tunasisitiza umuhimu wa kutumika zile kadi ambazo zinatumika kwenye mechi mbalimbali.

Tunajiuliza maswali kwa nini Morocco? Kwa nini waandishi waelezwe mabadiliko sasa? TFF ina nini? Mbona haikutujulisha kwamba siku tunajadili kwenye kikao ilikuwa tunapoteza muda?

Kwa misingi hiyo tunaandaa mkutano wa pamoja kati ya Taswa na wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali vya habari kesho ili tutoke na msimamo wa pamoja kuhusu TFF na hatua gani tuchukue kutokana na mambo haya ya waandishi wa michezo kutothaminiwa.

Tunawasisitiza wanachama wa Taswa waendelee kuwa watulivu kipindi hiki wakati tukitafuta ufumbuzi wa jambo hilo, lakini kwa kuanzia TASWA haikubaliani na utaratibu huu, hivyo TFF waufanye wenyewe kwa sababu wao ndio wenye mamlaka ya mpira na wanaona hatuna la kufanya na mawazo yetu huwa yanapuuzwa, kwani wametuomba tushirikiane nao kuandaa uataratibu wa tiketi hizo lakini hatutajiingiza huko maana kama hawakuheshimu kikao cha Agosti 17 itakuwa leo?

Hata kama TASWA itatoa mawazo mazuri namna gani, TFF haiwezi kuyafanyia kazi.Waendelee wenyewe na utaratibu wao maana kusudi haina pole.

Chama kimekuwa kikipokea shutuma nyingi kwa uamuzi unaotolewa na TFF sisi hatutaki tuwe kama yale mambo ya msafara wa ng’ombe, ambaye anayechelewesha yuko mbele,lakini viboko anapigwa wa nyuma ambaye ni TASWA. Hilo hatutalikubali hata kidogo.

Tunaishauri TFF iwe makini na jambo hili, vinginevyo heshima ya shirikisho hilo itaingia matundu bila sababu za msingi ni kama watu waliojificha mvua kwenye mpapai.

Tunamalizia kwa kusema kuwa kama TFF wenzetu wanajua mbio, sisi tunaelewa njia

Ahsanteni

Amir Mhando
katibu mkuu taswa

SERENGETI YAIMWAGIA CECAFA MILIONI 675!

Katibu Mkuu wa CECAFA Nicholas Musonye kushoto akipokea Mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 675 kutoka kwa Mkurungenzi Mkuu wa SBL Ajay Mehta kulia ni Caroline Ndungu Mkurugenzi wa Masoko SBL na katikati ni Meneja Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano SBL Teddy Mapunda. Kampuni ya bia ya serengeti ISBL) kupitiam bia yake ya Tusker itadhamini mashindano hayo kwa jumla ya shilingi miloni 675 za kitanzania kwa ajili ya kuendesha mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kugharamia tiketi za ndege kwa timu shiriki na maafisa wa CECAFA pamoja na marefa, malazi, usafiri wa ndani, uratibu, zawadi, ada mbalimbali, usalama, gharama za kutumia uwanja, usajili wa waandishi wa habari na gharama nyinginezo. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza tarehe 27 Novemba mpaka tarehe 11 Disemba mwaka huu ambapo mashindano hayo yanafanyika hapa nchini kwa mwaka huu. Maswhindano ya CECAFA mwaka huu yatashirikisha timu kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burubdi, Djibouti, Somalia, Ethiopia, Sudan, Tanzania, Zanzibar Eritrea na kwa mara ya kwanza CECAFA imeialika timu ya Ivory Coast kama timu mwalikwa wa mashindano hayo. SBL ndiyo mdhamini mkuu wa mashindano hayo ya CECAFA 2010 kupitia kinywaji chake cha TUSKER
Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa CECAFA Nicholas Musonye, Mkurugenzi wa Masoko SBL Caroline Ndungu na Teddy Mapunda Meneja Uhusiano na Mwasiliano SBL.

morocco ndani ya dar

Chamakh Mchezaji wa timu ya Asenal FC inayoshinriki Ligi Kuu Uingereza aliyekaa kulia ni akiwa na mchezaji mwenzaka mmoja wa wachezaji hatari wa timu hiyo aliyewasili pamoja na wachezaji wengine wa timu ya Taifa ya Moroco Kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K.Nyerere , Moroco iliyokuja kwa ndege ya Shirika la ndege la (KLM)inatarajiwa kuumana na timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars kwenye uwanja wa Taifa siku ya jumamosi.
Mchezo huo ambao ni wa kufuzu kucheza fainali za kombea la mataifa ya Afrika mwaka 2012 utaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha SuperSpot cha Afrika Kusini na watanzania wakae mkao wa kula siku ya jumamosi kwani tunaweza kuona burudani nzuri kama ilivyokuwa kwa Timu ya taifa ya Brazil,
hawa wakipiga stori mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K.Nyerere
Hapa wakislimiana na mmoja wa maafisa kutoka Ubalozi wa Moroco.
wachezaji wengine wakiendelea kutoka nje.
Mchezaji Chamakh wa timu ya Ligi Kuu ya Uingereza Asenal FC wa pili kuoka kulia akiongozana na wachezaji mwenzake kuingia kwenye basi tayari kwa kuelekea hotelini mara baada ya kuwasili jijini Dar es salaam usiku huu.
wakiendelea kutoka na kuingia kwenye basi lao.
Wachezaji mwa timu ya taifa ya Moroco wakipanda kwenye basi lililowachukua mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa J.K.Nyerere usiku wa jana

Oct 6, 2010

MIKUTANO YA MWAKA YA SHIRIKA LA FEDHA LA KIMATAIFA NA KUNDI LA BENKI YA DUNIA YAANZA.

Mikutano ya mwaka ya Bodi ya Magavana ya Shirika la fedha la Kimataifa na kundi la Benkiya Dunia kwa mwaka 2010 imeanza leo mjini Washington D.C. Kilele cha mikutano hiyo kitakuwa tarehe 8 - 10, mwezi Octoba 2010.

Bodi ya Magavana wa Shirika la Fedha la kimataifa ( Mfuko) na Bodi ya Magavana wa kundi la Benki ( Benki ) kwa kawaida hukutana mara moja kwa mwaka kujadili kazi za Taasisi zinazowahusu. Mikutano hii ya mwaka huwa inafanyika mwezi Septemba hadi Octoba, hufanyika mjini Washington kwa miaka miwili mfululizo na kwa mwaka wa tatu hufanyika kwa nchi mwanachama.

Uzinduzi wa Mikutano hii ya Bodi ya Magavana ulifanyika Savannah, Georgia, Amerika mwezi Machi mwaka 1946. Na mikutano ya kwanza ya mwaka ilifanyika mjini Washington mwaka1946.

Mwaka huu,Mikutano ya mwaka itaambatana pamoja na mikutano ya kimataifa ya kifedha na kamati za fedha, Kamati za maendeleo, kundi la nchi kumi, kundi la nchi ishirini na nne, na makundi mbalimbali ya nchi wanachama.

Aidha mwisho wa mikutano hii, Shirika la fedha la kimataifa, kamati ya mambo ya fedha, Kamati ya maendeleo pamoja na makundi mengine watapata nafasi ya kuwasiliana na kutoa mapendekezo yao.

Mikutano hii ya mwaka itaunganisha siku za utangulizi kabla ya ufunguzi rasmi kipindi ambacho Magavana watakitumia kwa kuzungumzia masuala ya kibiashara na kushauriana.Vilevile katika Mikutano hii ya mwaka, Bodi ya Magavana huwa inafanya maamuzi ya ni vipi mambo ya Fedha ya kimataifa yanapaswa kuwa na kukubaliana kuhusu maazimio husika.

Mikutanoya mwaka inakuwa na mwenyekiti ambaye ni Gavana wa Benki na wa Mfuko, na uenyekiti huo unakuwa ni wa kupokezana kati ya wanachama kila mwaka. Kila baada ya miaka miwili inachagua Mkurugenzi mtendaji. Kila mwaka wanachama wapya wowote wanakaribishwa katika Benki na mfuko.

Kwa sababu Mikutano hii ya mwaka inakusanya idadi kubwa ya wanachama kutoka nchi mbalimbali, hivyo shirika la fedha la kimataifa na kundi la Benki ya Dunia inatoa nafasi ya kuwapatia ushauri mkubwa na mdogo, kwa mpangilio wa kuwa na utaratibu maalumu au kutokuwa na utaratibu maalumu alimradi hawavurugi mpangilio uliopo.

Semina mbali mbali zinafanyika wakati wa mikutano na zinaaendeshwa na wafanyakazi wanachama kwa waandishi wa habari.Programu za Mikutano ya mwaka zimetengenezwa kwa kuzingatia matakwa ya sekta binafsi, wajumbe kutoka Serikalini na maafisa wakuu wa Mabenki na watumishi wa Mfuko.

Mikutano ya mwaka nje ya Amerika kuanzia mwaka

1947--2009

Mwaka Nchi
1947 London
1950 Paris
1952 Mexico City
1955 Istanbul
1958 New Delhi
1961 Vienna
1964 Tokyo
1967 Rio de Janeiro
1970 Copenhagen
1973 Nairobi
1976 Manila
1979 Belgrade
1982 Toronto
1985 Seoul
1988 Berlin
1991 Bangkok
1994 Madrid
1997 Hong Kong
2000 Prague
2003 Dubai
2006 Singapore
2009 Istanbul

Magavana wa mikutano hiyo ni Mawaziri wa fedha kutoka nchi mbalimbali, Magavana wa Benki kuu na Makatibu wa kuu wa Wizara za fedha.

Mpaka sasa karibu nchi zote zimeisha wasili katika mikutano hiyo.

Imetolewa na:

Ingiahedi Mduma

Msemaji Mkuu

Wizara ya Fedha na uchumi

Washington D.C

THE DON HIMSELF

Karibuni sana kwenye blog hii ya kijamii iliyosheheni makila kitu kuanzia siasa uchumi afya na burudani kwa ujumla wake.uingiapo kwenye blog hii ni mengi ambayo utapata nafasi ya kukutana nayo,kumbuka mawazo yako ndo hasa yanayojenga na kunifanya niwe na ufanisi zaidi.kariiiiiiibuuuuuuuuuuuu saaaaaaaaaaaaaaanaaaaaaaaaa.(THE DJ HIMSELF-JIWE)

Followers

BLOG ZA MARAFIKI

Search This Blog

ZILIZOPITA

DUNIA MUZIMA