Kipenga Chalenji chapulizwa leo Vumbi la Chalenji kuanza kutimka leo
|
Beki wa Kilimanjaro Stars,Shadrack Nsajigwa akichuana na mshambuliaji wa timu hiyo,salum Machaku katika mazoezi ya timu hiyo jana jijini Dar es salaam. PAZIA la michuano ya Kombe la Chalenji inafunguliwa leo jijini Dar es Salaam na kushirikisha timu 12 kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati na nyingine zilizoalikwa mahususi kuiongezea ladha michuano hiyo.
Michuano hiyo ya wiki mbili, mshindi wake ataibuka na dola 30,000 (karibu Shilingi 42 milioni) ambazo zimetolewa na wadhamini, Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL, ikishirikiana na ile ya Serengeti (SBL).
Timu hizo zimegawanywa katika makundi matatu, ambako Kundi A linaundwa na wenyeji Kilimanjaro Stars, Chipolopolo ya Zambia, Intamba ya Burundi na Somalia, ambayo haijawasili.
Kundi B linajumuhisha Amavubi ya Rwanda, wageni waalikwa, Ivory Coast, Sudan na Zanzibar Heroes wakati Kundi C linazo, Uganda Cranes, Harambee Stars ya Kenya, Flames ya Malawi na Ethiopia.
Kulingana na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), ambao ndio waandaaji wakishirikiana na shirikisho la soka nchini (TFF), wameeleza kuwa maandalizi yamekamilika.Kilimanjaro Stars leo watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Chipolopolo ya Zambia baada ya mchezo wa kwanza wa ufunguzi utakaoanza saa nane mchana utakazozikutanisha Somalia na Burundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholous Musonye alisema maandalizi yamekamilika na timu zote, isipokuwa Somalia tayari zilikuwa zimewasili nchini kusubiri kuanza kwa michuano hiyo.
Alisema mashindano haya kwa sasa yamezidi kuboreshwa na kuongezwa ladha kwani timu mwalikwa zimekuwa nyingi tofauti na miaka ya nyuma hali inayoonyesha kuonekana kutanuka kwa michuano hiyo mwaka huu.
Ufunguzi wa michuano hiyo utaanza saa 8:00 mchana kwa mchezo kati ya Burundi na Somalia ambao utafanyika kabla ule wa wenyeji, Kilimanjaro Stars dhidi ya Zambia.
Michezo hiyo itatanguliwa na sherehe za ufunguzi ambapo timu zote 12 zitaingia kwa maandamano maalum na kufunguliwa rasmi kwa mashindano hayo.
Kwa upande wa kikosi cha Kilimanjaro Stars chini ya kocha wake Jan Poulsen kiko kamili tayari kwa mchezo wao wa kwanza dhidi ya Chipolopolo huku wakitamba kuwa watahakikisha wanaanza vyema kuipeperusha bendera ya nchi na kulibakiza kombe hilo hapa nyumbani.
Huo utakuwa mtihani wa kwanza kwa kocha huyo (Poulsen) katika mashindano hayo makubwa baada ya kukabidhiwa mikoba na Marcio Maximo mapema mwaka huu.
Kibarua hicho kitanoga endapo ataanza vyema kazi yake kwa kuipa ushindi Kilimanjaro Stars katika michuano hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi, Poulsen alisema wamejiandaa vyema katika mashindano hayo na anategemea vijana wake wataanza kazi yao kama alivyowaagiza kwa kuanza na ushindi katika mchezo wa leo hivyo ni matumaini yake watakua katika nafasi nzuri ya kulitwaa kombe hilo.
Baadhi wa wachezaji wa kikosi cha Kilimanjaro Stars ambacho jana kilikuwa kikifanya maandalizi yake ya mwisho kimetamba kuwa kitahakikisha kinatoa dozi kwa wapinzani wao mara wanapokutana ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kufika katika hatua ya fainali.
Nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alisema wamejiandaa kupigana hadi tone la mwisho katika mashindano hayo ili kuiletea sura mpya ya maendeleo Tanzania katika soka na kuhakikisha inabakiza kombe hilo hapa nyumbani.
Kocha wa Zambia, Dario Boneti amesema hatishwi na ugeni dhidi ya wapinzani wao katika mchezo huo wa kufungua pazia hilo bali anaamini ndio ataanza kurusha karata yake na kuhakikisha anashinda ili kuiwezesha kusonga mbele.
Wakati huohuo, Sweetbert Lukonge anaripoti kuwa huenda ratiba ya michuano ya Chalenje ambayo inaanza leo ikabadilishwa kufuatia kuwepo kwa wasiwasi juu ya ushiriki Somalia katika michuano hiyo.
Timu hiyo ambayo ilitarajiwa kuingia nchini jana tayari kwa kushuka uwanjani leo jioni katika mchezo wa pili wa ufunguzi wa michunao hiyo dhidi ya Burundi sasa inatarajiwa kuwasili nchini leo.
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Msonye alisema kuwa kutoka na hali hiyo kamati ya mashindano ya baraza hilo ingekutana jana jioni kwa lengo la kuhakikisha mechi ya pili ya ufunguzi inakuwepo kama ilivyopangwa hata kama Somalia isiposhiriki.
"Mpaka sasa karibu timu zote zimewasili nchini tayari kwa michuano hiyo isipokuwa Somalia na Ethiopia.
"Lakini, pamoja hayo tuna wasiwasi juu ya ushiriki wa Somalia kwani kwa taarifa zilizotufikia timu hiyo ambayo ilikuwa iwasili leo,jana, sasa itawasili kesho,leo.
"Kutokana na hali hiyo tutakutana baadaye ili kuangalia ni jinsi gani ya kufanya ili mechi ya pili iweze kuwepo, " alisema Musonye chanzo mwananchi |
THE DON HIMSELF
Karibuni sana kwenye blog hii ya kijamii iliyosheheni makila kitu kuanzia siasa uchumi afya na burudani kwa ujumla wake.uingiapo kwenye blog hii ni mengi ambayo utapata nafasi ya kukutana nayo,kumbuka mawazo yako ndo hasa yanayojenga na kunifanya niwe na ufanisi zaidi.kariiiiiiibuuuuuuuuuuuu saaaaaaaaaaaaaaanaaaaaaaaaa.(THE DJ HIMSELF-JIWE)
No comments:
Post a Comment