HALI imeendelea kuwa mbaya kwa vigogo wa soka duniani baada ya Ufaransa kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mexico, huku kiungo wa Nigeria, Sani Kaita akiomba msahama kwa mashabiki kwa kitendo chake kilichoighalimu timu yake kufungwa 2-1 na Ugiriki.
Hakuna aliyeamini kilichokuwa kinatokea kwenye Uwanja wa Polokwane ambako kulishudia miamba mabingwa wa Dunia 1998 wakiendeshwa mchamchaka na vijana wa Mexico walionekana kujipanga na kufanya watakalo katika dakika zote tisini.
Mexico iliyotawala mchezo huo iliandika bao lake la kwanza dakika 63, kupitia kwa Javier Hernandez aliyevunja mtego wa kuotea uliowekwa na mabeki wa Ufaransa waliokosa ushirikiano katika muda wote wa mchezo huo.
Beki Erick Abidal alimwangusha Pablo Barrera kwenye eneo la hatari na ambayo mwamuzi kutoka Saudi Arabia aliamuru penalti iliyofungwa na Cuauhtemoc Blanco dakika ya 78 na kumaliza kabisa matumaini ya Ufaransa ya kupata sare kwenye mchezo huo.
Kwa matokeo hayo sasa Ufaransa imeungana na wenyeji Afrika Kusini kujiandaa na safari za kuaga mashindano hayo mapema, kwani watalazimika kuomba Mexico na Uruguay zitoke sare ili zifungwe ili iweze kufuzu.
Kiungo wa Nigeria, Kaita ameomba msamaha kwa watu wote barani Afrika kwa kitendo chake kilichosababisha kupewa kadi nyekundu iliyowasaidia Ugiriki kupata ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa Kundi B uliochezwa Uwanja wa Free State jana.
"Naomba msamaha kwa kila moja. Watu wa Nigeria, viongozi na wachezaji wenzangu," alisema kiungo huyo mwenye miaka 24 mbele ya wanahabari baada ya kutolewa kwa kitendo chake kutaka kumkanyaga mchezaji mwenzake.
Huku Super Eagles wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa kwa mpira wa adhabu ya Kalu Uche walionekana kutawala mchezo hadi pale Kaita alipofanya kitendo cha kipuuzi cha kumkanyaga Vassilis Torosidis dakika ya 33 na kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Kiungo huyo anayecheza soka yake nchini Russia aliondoka uwanjani hapo akiwa amejifunika uso wake kwa jezi, na kufanya mchezo huo kubadilika kabisa na Ugiriki kutawala zaidi.
Dakika 11 baadaye Ugiriki walisawazisha kupitia kwa Dimitris Salpingidis na kuipa nchi yake bao la kwanza katika historia yao ya Kombe la Dunia na walifanikiwa kupata bao la pili zikiwa zimebaki dakika 20 lililofungwa na Torosidis.
"Nakubali na uamuzi wa kupewa kadi nyekundu, nimeuzunika kwa kitendo changu, natumaini Argentina itaweza kutusaidia," aliongeza Kaita ambaye atakosa mechi ya mwisho ya kundi hilo.
Ushindi wa Ugiriki umewafanya kufikisha pointi tatu sawa na Korea Kusini, ambayo imefungwa kwa mabao 4-1 na Argentina mapema jana, huku Nigeria ikishikiria mkia bila ya pointi baada ya mechi mbili.
Nigeria, moja ya nchi zilizotegemewa na Afrika kufanya vizuri kwenye fainali hizo, sasa watalazimika kushindi dhidi Korea Kusini hapo Juni 22 mjini Durban na kuomba Ugiriki ifungwe na Argentina mjini Polokwane ili waweze kufuzu kwa hatua ya pili.
Lakini hali hiyo imeonekana kutomshitua mkongwe Nwankwo Kanu ambaye anaamini bado nchi yake ina nafasi ya kusonga mbele.
"Kama ukiangalia jinsi kundi lilivyo uwezi kuwa na wasiwasi sana, lakini tunachotakiwa kwetu ni kushinda," alisema.
"Hatuwezi kwenda tukiwaza sare, tunachotakiwa ni kushinda na kuomba kwa dua zote Argentina ikiendeleze makali yake kwa kuifunga Ugiriki."
No comments:
Post a Comment