
WANAHARAKATI wa mashirika yasiyo ya kiserikali wametoa mapendekezo ambayo wanataka yatekelezwe na vyama vya siasa vinavyogombea kuingia madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu.
Hivi karibuni, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea Haki za Binadamu, Jinsia na Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct) ulizindua Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Ilani hiyo imetathmini utendaji wa serikali iliyoko madarakani kwa kipindi cha miaka mitano na kuweka mapendekezo mengineyo.
Katika tathmini ya Ilani ya mwaka 2005 mambo kadhaa yameainishwa kama kipimo cha utekelezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne.
Ilani hiyo inadai kuwepo kwa jitihada za kukuza uchumi kwa mtazamo wa haki sawa, kuondoa matabaka yanayojitokeza, kupambana na mifumo kandamizi na ubaguzi hususan ule wa kijinsia na kuwepo kwa mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanawake wapiga kura wanashiriki katika kuzalisha mali na maamuzi muhimu ya maendeleo ya taifa lao pamoja na kunufaika na matunda ya jasho lao.
Katika tathmini hiyo wanaharakati wamesifia kukua kwa uchumi, lakini wamelaumu utegemezi wa wahisani uliosababisha kukua huko kutodumu:
“Katika kipindi hiki cha miaka mitano, tulishuhudia kukua kwa uchumi kama ilivyotarajiwa katika Mkukuta. Kwa mfano, kwa kutumia kigezo cha Pato la Taifa (GDP) kulikuwa na ongezeko la Pato la Taifa kutoka asuilimia 6.7 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2008. Hata hivyo, sura ya matokeo ya mfumo tegemezi wa uchumi wetu na jinsi tulivyomezwa na mfumo wa utandawazi.”
Ilani hiyo pia inamulika umasikini uliokithiri licha ya kukua kwa Pato la Taifa. Kwa mfano, asilimia ya watu walio masikini kupindukia ilipungua kidogo tu, kutoka asilimia 35.7 mwaka 2004 hadi asilimia 33.2 mwaka 2007. Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi halisi ya Watanzania walio masikini kupindukia iliongezeka kutoka asilimia 11.4 mwaka 2001 hadi kufikia asilimia 12.9 mwaka 2007.
Kuhusu suala la ajira, Ilani hiyo imeonyesha kuwa idadi ya Watanzania walioajiriwa na kujiajiri imeongezeka. Inasema kuwa takriban asilimia 87 ya Watanzania wenye umri wa miaka 15 na zaidi wameajiriwa na asilimia mbili ya kundi hili haina ajira. Hii ni pamoja na asilimia 90.5 ya wanaume na 88.9 ya wanawake.
Nini basi chanzo cha umasikini wa kupindukia kama Watanzania walio wengi wana ajira? Ilani hiyo inabainisha kuwa asilimia 67.2 ya ajira zote ni zile za kujiajiri wenyewe ama kwenye mashamba madogo au katika sekta isiyo rasmi.
“Wengi walioajiriwa au kujiajiri kwenye mashamba au sekta isiyo rasmi wanaishi maisha magumu yasiyo na kipato cha uhakika na kisichotosha. Wengine hasa wanawake, vijana na watoto hawalipwi mshahara wowote kwa kazi au huduma wanayotoa,” wanasema wanaharakati katika ilani yao.
Kwa upande mwingine ilani hiyo inabainisha kuwa sekta rasmi nchini inaajiri asilimia 10 tu ya Watanzania huku wakilipwa mishahara midogo isiyokidhi mahitaji ya msingi ya wafanyakazi. Hiyo nayo ni sababu nyingine inayotajwa kama chanzo cha umasikini uliopindukia.
Licha ya umasikini, ilani hiyo inabainisha kuwepo kwa ongezeko la matabaka. Utafiti unaonyesha kuwa wanaume wana mishahara mikubwa kuliko wanawake. Kwa mfano, utafiti wa Baraza la Taifa la Takwimu mwaka 2006, unaonyesha kuwa, mshahara wa mwanamume mwenye miaka 15 na kuendelea, ulikuwa ni Sh50,000 kulinganisha na Sh32,000 za mwanamke katika umri huo huo.
Aidha matabaka pia yanajitokeza kwenye suala la elimu. Wasio na elimu wanalipwa mishahara midogo. Ilani hiyo imetoa mfano wa pato la mfanyakazi mwenye elimu ya sekondari na zaidi kuwa ni Sh207,433 kulinganisha na Sh40,134 kwa wale ambao hawakwenda shule. Kwa wale waliojiajiri pato lao ni Sh129,494 kwa wenye elimu ya sekondari huku wasio na elimu wakiambulia Sh 48,920.
Katika sera ya uwekezaji, ilani hiyo inaonyesha jinsi serikali ilivyojikita katika kugawa rasilimali za Taifa kwa wageni bila kujali wazawa... “Katika kipindi cha miaka 10, sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yetu imechukuliwa na wawekezaji, wengi wao ni makampuni makubwa ya nje. Si ardhi tu, bali pia maji, madini, misitu, wanyama pori na samaki."
“Wananchi walio wengi wamehamishwa kutoka makao yao kwa nguvu, wanakosa nafasi kwa uzalishaji katika kilimo, ufugaji na uvuvi na wengine wanapambana na maradhi yanayotokana na uchumi za makampuni.”
Ilani mpya
Katika kutoa madai mapya, Ilani ya mwaka 2010 imekuja na madai mapya ikiyaweka katika makundi tofauti yaani serikali, vyama vya siasa, wagombea na asasi za kiraia.
Kwa upande wa serikali, Ilani hiyo imeitaka kusimamia kwa uadilifu matumizi ya rasilimali za taifa letu, ili zitumike kwa manufaa ya Watanzania wote. Vilevile, serikali inapaswa kusimamia utawala bora na uwajibikaji kwa mtazamo wa kijinsia.
Katika masuala ya uchaguzi, serikali imetakiwa kudhibiti matumizi ya mabaya ya fedha za uchaguzi na kuhakikisha fedha zote za umma zitakazotumika katika uchaguzi zinawafikia wanawake kama wapiga kura na wagombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Ilani hiyo pia imeitaka serikali kutenga kipindi maalumu kwa wagombea wote kwenye vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali kwa ajili ya kampeni. Serikali pia imetakiwa kusimamia taratibu za kupiga kura ili kuhakikisha kuwa taratibu hizo haziathiri makundi maalumu.
“Ukomo wa wanasiasa kukaa madarakani uwe ni awamu mbili tu. Isitoshe, wanasiasa wasiwe na vyeo zaidi ya kimoja. Kwa mfano, mkuu wa mkoa, waziri, mbunge na wengineo ili kuepusha mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao.”
Kwa upande wa vyama vya siasa, ilani hiyo imebainisha kuwa ni mhimili mkuu wa demokrasia shirikishi na ya ushindani inasema ni lango kuu la kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi na hatimaye katika nafasi muhimu za uongozi wa taifa.
Hata hivyo, wanaharakati katika Ilani hiyo wanasikitishwa na jinsi mfumo dume unavyotumika katika vyama vya siasa... “Vyama vimewatumia wanawake na baadhi ya vijana kama wapiga debe, wahamasishaji na wasindikizaji katika mchakato wa uchaguzi. Wanawake wengi wanaposimama kama wagombea vyama vinawatupa na kuwaweka pembezoni.”
Ilani hiyo inavilaumu vyama vingi kwa kushindwa kuleta usawa wa kijinsia badala yake vimezidi kuimarisha utamaduni wa ubaguzi dhidi ya wanawake.
“Tunadai vyama vya siasa viache kuwarubuni wanawake kwa kutumia ‘Viti maalumu’ ambavyo hatima yake ni kuwapa wachache waliovipigia debe fursa ya kuchaguzliwa na kuingia katika vyombo vya uwakilishi wa maamuzi katika ngazi duni.”
Kwa upande wa wagombea, wanaharakati wanawataka kutotumia nguvu ya fedha kununua kura bali watumie busara na nguvu ya hoja kushawishi wapiga kura.
Wagombea pia wasitumie lugha za matusi au ubabe wa kudhalilisha wanawake na wasirubuni wananchi kwa kuwaahidi ahadi zisizotekelezeka... “Kiongozi kama huyo ni sumu kwa taifa letu, ni sumu kwa demokrasia na ni sumu kwa makundi ya wanawake na wanaume yanayotaabika kutokana na rasilimali za taifa kutowafikia.”
Kwa upande wa asasi za kiraia, Ilani hiyo inazitaka asasi hizo kuwatetea wanawake kwa kuwahamasisha kugombea nafasi za uongozi na kukataa kuburuzwa kama wapiga debe au kurubuniwa kwa kupewa ‘nafasi za upendeleo’.
No comments:
Post a Comment