Jun 9, 2010

BAADA YA BABU CHUCHU SASA OLIVER NGOMA NAYE HATUNAYE


Katika hali ambayo bado sijaielewa,jana jioni nilikuwa nikijaribu kutengeneza orodha ya wanamuziki au miziki 100 maarufu ama kwa lugha nyingine, iliyotamba sana barani Afrika(Africa’s 100 Top Hit Songs). Nilichoamua kukifanya ni kujaribu kwenda(kwa kutumia mtandao) nchi moja mpaka nyingine huku nikijaribu kuchunguza kama nchi hiyo ina mwanamuziki au muziki ambao ulitokea kutamba zaidi barani Afrika.

Zoezi hilo bado naendelea nalo.Kwa hakika ni zoezi gumu hususani ukizingatia jinsi bara la Afrika lilivyosheheni vipaji na wasanii wa kiwango cha kimataifa.Nani aingie katika Top 100 na nani abakie nje.Mashabiki wake hawatonilalamikia kwanini nimemuweka pembeni mtu wao?Mawazo kama hayo yalitawala.

Wakati naendelea na zoezi hilo,nikawa pia napitiwa na huzuni kila nilipokuwa nasoma na huku nikisikiliza muziki kutoka kwa mwanamuziki fulani ambaye alishaiga dunia.Wapo wengi ila nazikumbuka hisia zangu nilipoyapitia majina kama Mbaraka Mwaruka Mwinshehe(Tanzania),Franco(DRC Congo),Madilu System(DRC Congo),Brenda Fassie(Afrika Kusini),Miriam Makeba(Afrika Kusini),Lucky Dube(Afrika Kusini),Fella Kuti(Nigeria) na kadhalika na kadhalika.

Nilipofika Gabon,jina ambalo bila shaka sote tunakubaliana kwamba ni vigumu(kama sio kashfa kabisa) kuliacha katika orodha ni jina la Oliver N’goma. Ni jana hiyo nilipojikuta nikisikiliza nyimbo kadhaa za Oliver N’goma kama vile Lusa,Bane,Betty,Nge’ Adia,Icole nk.Nikakumbuka sana jinsi nyimbo zake, zilivyotokea kuwa nyimbo ambazo haziwezi kukosa kunako shughuli mbalimbali hususani harusi hapa Bongo.Kwangu mimi Oliver alikuwa ni mfalme wa aina yake katika Zouk barani Afrika.

Unaweza kupata picha ya jinsi nilivyopata mshtuko na masikitiko kuamka asubuhi na kusikia kwamba Oliver N’goma amefariki dunia! Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, Oliver N’goma au Noli kama alivyojulikana huko kwao Gabon, amefariki kwa ugonjwa wa figo (kidney failure) akiwa hospitalini alikokuwa amelazwa.

Oliver alizaliwa tarehe 23 March mwaka 1959 katika mji unaoitwa Mayumba uliopo Kusini Magharibi mwa Gabon. Alizaliwa katika familia ambayo haikuwa ngeni katika masuala ya muziki. Baba yake alikuwa mpiga kinanda cha mdomo(harmonica) maarufu.Mwanzoni mwa maisha yake alipenda sana kuwa mpiga picha.Baadaye aliikacha taaluma hiyo na kuendelea na muziki kitu ambacho kilikuwa kwenye damu.

Mwishoni mwa miaka ya 80 ndipo alipotoa albamu yake iliyobeba jina Bane ambayo ndio ilikuwa chanzo cha umaarufu na mafanikio makubwa katika safari yake ya muziki.Rest In Peace Oliver N’goma.


No comments:

THE DON HIMSELF

Karibuni sana kwenye blog hii ya kijamii iliyosheheni makila kitu kuanzia siasa uchumi afya na burudani kwa ujumla wake.uingiapo kwenye blog hii ni mengi ambayo utapata nafasi ya kukutana nayo,kumbuka mawazo yako ndo hasa yanayojenga na kunifanya niwe na ufanisi zaidi.kariiiiiiibuuuuuuuuuuuu saaaaaaaaaaaaaaanaaaaaaaaaa.(THE DJ HIMSELF-JIWE)

Followers

BLOG ZA MARAFIKI

Search This Blog

ZILIZOPITA

DUNIA MUZIMA